NEWS

Monday, 29 November 2021

TNDF yajengea wanawake, vijana uwezo wa kukabiliana mabadiliko ya tabianchi




BAADHI ya wanawake na vijana kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wamepata mafunzo ya kusaidia kujenga ustahimilivu wa jamii katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo yao na Taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo yametolewa na Jumuiko la Asasi Zisizo za Kiserikali katika Bonde la Mto Nile nchini Tanzania (TNDF), jijini Mwanza wiki iliyopita kwa siku tano mfululizo kwa kila kundi lenye washiriki 35.



Akifungua mafunzo hayo kwa wanawake na baadaye kwa vijana, Mwenyekiti wa TNDF, Dkt Donald Kasongi amesema mabadiliko ya tabianchi kwa sasa hayakwepeki, hivyo ni muhimu kuwa na mbinu za kukabiliana na athari zake katika jamii.



“Tumeelekeza mafunzo haya kwa wanawake na vijana kwa kuzingatia kuwa ndio makundi muhimu katika ujenzi wa Taifa, lakini pia ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dkt Kasongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiko la Asasi Zisizo za Kiserikali katika Bonde la Mto Nile (NBDF) linaloundwa na nchi 10, lenye makao makuu Entebbe nchini Uganda.


Dkt Kasongi akifungua mafunzo hayo kwa vijana

Dkt Kasongi amesema mabadiliko ya tabianchi, hasa ukame na mafuriko yana athari kubwa kwa rasilimali maji ambayo ni muhimu kwa uzalishaji wa chakula na nishati ya umeme katika nchi zilizopo Bonde la Mto Nile, ikiwemo Tanzania.

“Tunatarajia na kutamani kuona wanawake na vijana waliohudhuria mafunzo haya wanakwenda kuwa walimu na chachu muhimu ya kusaidia jamii kujenga ustahimilivu katika maeneo yao kuhusiana na maji, hasa kukabiliana na majanga ya ukame na mafuriko,” Dkt Kasongi amesema.



Mratibu wa TNDF, Hadija Malimusi amebainisha kuwa wanawake na vijana waliopata mafunzo hayo ni kutoka asasi zaidi ya 20 ambazo ni wanachana wa Jumuiko hilo.

Hadija ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika juhudi za kusaidia jamii kujenga uwezo wa kujihami dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo ni pamoja na ongezeko la mgao wa huduma za maji na umeme.


Kwa upande wake, Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Samson Msilu kutoka Chuo cha Uongozi wa Serikali za Mitaa Dodoma, amesema washiriki hao wamepata uwezo na utayari wa kusaidia kujenga ustahimilivu wa jamii na kuimarisha jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Bonde la Mto Nile.


Msilu akitoa mada

Nao washiriki wa mafunzo hayo, wakiwemo Josephine Mihama, Fadhila Ndegeya na Emmanuel Isaya wameishukuru TNDF, wakisema imewajengea uwezo wa kuwa mabalozi na wahamasishaji wa mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika jamii.


“Mafunzo haya yametumepatia mwanga, tumejifunza kwamba wanawake tuna wajibu na nafasi kubwa katika kusaidia kuelimisha jamii umuhimu wa kutunza mazingira ya Bonde la Mto Nile kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo,” amesema Josephine kutoka taasisi ya Governance Links ya jijini Mwanza.

Naye Fadhila kutoka Karagwe mkoani Kagera, ameahidi kwenda kuelekeza nguvu kubwa katika kuhamasisha jamii juu ya upandaji miti kwa wingi, utunzaji vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.


Siku ya mwisho ya mafunzo ya hayo kila kundi limepelekwa wilayani Magu, Mwanza kujifunza kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kujionea maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, hasa mafuriko na ukame, na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na majanga hayo.




(Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages