NEWS

Friday 10 December 2021

AICT Mara na Ukerewe yaendeleza uhamasishaji elimu jumuishi kwa watoto



KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na taasisi ya Right to Play, limeendelea kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kutoa elimu jumuishi kwa watoto, wakiwemo wenye mahitaji maalumu.

Uhamasishaji huo umefanyika sambamba na bonanza la michezo mbalimbali wiki iliyopita, katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyansangero iliyopo kata ya Nyamwaga wilayani Tarime, walengwa wakiwa ni wanafunzi wa awali na darasa la kwanza hadi la nne.



Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota ameihimiza jamii kutowaficha ndani watoto wenye ulemavu au mahitaji maalumu, ili kuwawezesha kujumuika na wengine, kwani wana haki ya kuendelezwa na kunufaika na fursa zinazowazunguka.

“Tuelewe kwamba hawa watoto ni watoto kama watoto wengine na pia wana haki ya kupata elimu na kuendelezwa katika vipaji vyao,” Rebeca amesema.


Rebeca akizungumza

Rebeca amesema kuwapatia watoto wenye ulemavu nafasi kutasaidia pia kupunguza utegemezi katika jamii na hawataonekana mizigo kwenye familia, au jamii.

“Yafaa kwanza tuwapende, tuwathamini, tuwasikilize na kuwashirikisha katika maamuzi kuanzia ngazi ya familia, maana kwa kufanya hivyo kutawafanya kujiona kama sehemu ya jamii na kutawaepusha na mila potofu au kandamizi,” Ofisa Mradi huyo amesema.


Mwalimu Sophia Range na Rebeca wakikabidhi kombe kwa washindi

Kwa upande wake, mgeni rasmi wa bonanza hilo, Afisa Elimu Kata ya Nyansincha, Mwalimu Sophia Range amesisitiza umuhimu wa ujumuishwaji katika elimu na ufundishaji bora, ambapo ni jukumu la wazazi, walezi na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa hayo yanazingatiwa.

“Wazazi na wanafunzi wa Nyansangero, uwezo tunao, sababu tunayo na nia tunayo ya kuboresha elimu na pia ya kutokomeza ujinga katika eneo letu la Nyansangero,” Mwalimu Sophia amesema.

Aidha, amewataka wanafunzi kuacha utoro shuleni na kuwasihi wazazi kuwapa ushirikiano wadau wa elimu wanaokuja kwa nia ya kuinua maendeleo ya elimu katika maeneo yao.


Katika bonanza hilo, wanafunzi wamechuana katika michezo mbalimbali, ikiwemo kuvuta kamba, kukimbia kwa magunia, kusoma, mpira wa pete, kibao fumbo na mpira wa miguu kwa wavulana. Washindi wamekabidhiwa zawadi mbalimbali.

(Habari na picha: Geofrey John wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages