Dkt Halfan Haule |
MITI 1,200 imepandwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kwangwa, ikiwa ni sehemu ya maonesho ya kimataifa ya kilimo mseto, yaliyofanyika kwa siku tatu mfululizo mjini Musoma, Mara.
Akizungumza wakati wa kufunga maonesho hayo jana Desemba 4, 2021, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Halfan Haule alipongeza Shirika la Maendeleo la VI-Agroforestry lenye makao makuu nchini Sweden, kwa kudhamini maonesho hayo.
“Pia kupitia mashirika yaliyopo mkoani Mara, miti milioni 1.5 imepandwa na zaidi ya milioni 2.121 imepandwa katika maeneo mbalimbali nchini,” DC Haule amesema.
Dkt Haule pia amekabidhi vyeti kwa mashirika 16 yaliyoshiriki na zawadi mbalimbali kwa mashirika na taasisi zilizofanya vizuri zaidi katika maonesho hayo.
Kwa upande wake, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Patrick Gumbo amesema udhamini wa shirika la VI-Agroforestry katika kilimo mseto umesaidia wananchi wa kawaida kwa kuwapa elimu inayowawezesha kuhifadhi mazingira huku wakijipatia kipato na uhakika wa chakula.
Amependekeza maonesho hayo yawe sehemu ya vyanzo vya Serikali kupata taarifa zitakazowesha sera mbalimbali, zikiwemo za kuweka ulinganifu kati ya mauzo na gharama zinazotumiwa na wakulima ili kuwaepushia unyonyaji.
“Na sisi wengine katika serikali za mitaa, maonesho haya yawe sehemu ya kutufanya tuone ni jinsi gani tunakwenda kutunga sheria za kumwezesha mwananchi wa kawaida kuzalisha na kupata mapato kwa mujibu wa nguvu alizotumia,” Meya Gumbo amesema.
(Imeandikwa na Mara Online News, Musoma)
No comments:
Post a Comment