
Askofu wa SDA Jimbo la North Mara Field, Dkt. Benjamin Ngalama Biha (aliyevaa joho), katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kulia kwa Askofu) wakati wa tafrija ya kumpongeza kwa kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa.
Tarime
---------------
Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Jimbo la North Mara Field limempongeza Askofu wa jimbo hilo, Dkt. Benjamin Ngalama Biha, kwa kuhitimu na kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa.
Tafrija ya kumpongeza Askofu Dkt. Ngalama ilifanyika mjini Tarime jana Jumapili, na kudhuriwa na waamini wa dhehebu hilo kutoka wilaya za Tarime, Serengeti na Rorya zinazounda jimbo hilo.

Askofu Dkt. Ngalama na mke wake wakikata keki katika tafrija hiyo.
Akizungumza katika tafrija hiyo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele aliyekuwa mgeni rasmi, alimpongeza Askofu Dkt. Ngalama na kumuahidi ushirikiano katika kuendelea kulinda na kudumisha amani kwa maendeleo ya wilaya hiyo.
"Nikupongeze sana, ulichotueleza unatufundisha kuwa katika maisha lazima tuwe na uzalendo wa kuyasimamia yale tuliyachagua na tufike sehemu sahihi," alisema Meja Gowele.

Wanafamilia wakimkabidhi Askofu Dkt. Ngalama zawadi katika tafrija hiyo.
"Sisi kama serikali tutafanya kazi na wewe, ni matarajio yangu utatusaidia kutatua changamoto ndani ya kanisa na kutatua migogoro kwenye jamii,” alisema Meja Gowele na kuendelea:
"Naomba sana wana-Tarime tusimamie amani na utulivu, bila amani tusingekuwa hapa, wachungaji nawashukuru kwa namna mnavyoiunga mkono serikali katika kutatua changamoto mbalimbali na kuilea jamii kiimani.”

Askofu Dkt. NGalama akipokea zawadi ya fedha katika tafrija hiyo.
Awali, Askofu Dkt. Ngalama akielezea safari yake ya elimu aliwahimiza waamini kusomesha watoto wao na kutowakatisha tamaa ili waweze kutimiza njonzi zao katika maisha yao.
"Tusiwakatishe tamaa wanaosaka harakati za kusoma, kila niliyekutana naye alisema ‘wewe huwezi usijaribu’, mambo hata kama ni magumu kiasi gani usije ukakata tamaa.
"Mwamini Mungu atakusaidia, usikatishe njonzi zako, tuzidi kuwa wanyenyekevu kuliko tulivyokuwa mwanzo,” alisema Askofu Dkt. Ngalama.

Sehemu ya viongozi waalikwa wakifurahia jambo katika tafrija hiyo.
Aidha, Askofu Dkt. Ngalama alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wao kama viongozi wa dini wataendelea kuwa mabalozi wa amani kwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano kwa manufaa ya wilaya ya Tarime na Taifa.

Sehemu ya waamini wakifuatilia jambo katika tafrija hiyo

Sehemu ya waamini wakiwa katika tafrija hiyo

Askofu Dkt. Ngalama katika picha ya pamoja na familia yake wakati wa tafrija hiyo.

Askofu Dkt. Ngalama na mke wake (waliokaa) katika picha ya pamoja na kamati iliyoandaa tafrija hiyo.
No comments:
Post a Comment