NEWS

Wednesday 8 December 2021

Mfuko wa Maji wawezesha uwekaji vigingi 240 bwawa la Manchira



BODI ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imeishukuru Wizara ya Maji kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa, kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutengeneza vigingi vya kuonesha mipaka ya bwawa la maji la Manchira wilayani Serengeti, Mara.

Shukurani hizo zimetolewa leo na Ofisa wa LVBWB katika ofisi ya Musoma, Mhandisi Mwita Mataro wakati wa shughuli ya kupanda miti 10,000 katika hifadhi ya bwawa hilo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, yatakayofikia kilele kesho Desemba 9, 2021.

“Tumeweka vigingi 240 kuzunguka bwawa ili kuonesha mipaka halisi ya hifadhi ya bwawa, kazi hii imefadhiliwa na Mfuko wa Maji wa Taifa,” Mhandisi Mataro amesema.


Mhandisi Mataro (kushoto mbele) akitoa taarifa fupi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi (mwenye viatu vyeupe mbele)

Mhandisi Mataro ametaja vikwazo vinavyolikabili bwawa la Manchira kuwa ni uchimbaji mchanga na moramu ndani ya hifadhi ya bwawa, hasa katika kijito cha Kebosongo.

Vikwazo vingine amesema ni ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya kuni, mkaa na kuchomea matofali, mifugo kuingia, njia zinazokatiza na uchomaji moto ndani ya hifadhi ya bwawa hilo.



Hata hivyo, Mhandisi Mataro ametaja hatua zilizochukuliwa kukabiliana na hali hiyo kuwa ni pamoja na Bodi kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yote ya Vitongoji, vijiji na kata zinazozunguka bwawa la Manchira.

Pia, kusimika mabango 10 ya katazo la shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya bwawa, kujenga kituo cha kuchukulia takwimu kwenye bwawa na upandaji wa miti 10,000 kwenye hifadhi ya bwawa hilo.



Katika maadhimisho hayo ya miaka 60 ya Uhuru, MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi ameongoza viongozi mbalimbali wa chama na Serikali, wadau na wananchi kupanda miti katika hifadhi ya bwawa la Manchira.

RC Hapi ametumia nafasi hiyo pia kuhimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji na kutaka wanaokata miti na kuingiza mifugo katika vyanzo vya bwawa hilo kupewa adhabu kali.


RC Hapi akipanda mti

“Miti hii itunzwe kama kielelezo cha maadhimisho ya miaka 60 na Uhuru. Adhabu ya kuingiza ng’ombe iwe ni kupanda miti 100, kuwepo na mkakati wa kuweka uzio katika bwawa hili na kila kaya ipande angalau miti mitano kwenye chanzo cha maji,” ameagiza.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages