NEWS

Saturday 4 December 2021

Utekelezaji mradi wa maji Mugango-Kiabakari: Wananchi Musoma Vijijini kupewa kipaumbele, wamshukuru Rais Samia, Mbunge Muhongo



Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo.

WAKAZI wa kata za Mugango na Tegeruka katika jimbo la Musoma Vijijini, watapewa kipaumbele cha kunufaika na mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari unaotekelezwa wilayani Butiama, imeelezwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Mugango-Kiabakari, Mhandisi Cosmas Sanga, mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 75 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mradi huu utanufaisha wananchi 164,900 wa majimbo ya Musoma Vijijini na Butiama. Awamu ya kwanza itanufaisha kata ya Mugango na baadaye kata ya Tegeruka,” Mhandisi Sanga amewambia wanahabari Musoma Vijijini, hivi karibuni.

Baadaye mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2020, utasambaza maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kwa wakazi wa vijiji vya Kurwaki, Kiriba na Bwai Kumsoma, amesema.

Wakazi wa maeneo yatakayonufaika na mradi huo Musoma Vijijini, wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia, wakisema mradi huo utawaondolea kero ya miaka mingi ya kutembea umbali mrefu kwenda ziwani kuchota na kutumia maji yasiyo salama.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwibara, John Waitare amesema wananchi wameupokea mradi huo kwa mikono miwili. “Wanafurahia sana,” amesema.

Mkazi wa kijiji cha Mugango, Mafuru Marambo amesema “Ninawashukuru viongozi wetu, nina imani huu mradi utamtua mama ndoo kichwani kama ilani ya CCM inavyosema.”

Marambo ameongeza “Tunamshukuru Mbunge wetu, Profesa Sospeter Muhongo kwa sababu naye amefanya jitihada kubwa za ufuatiliaji hadi mradi huu umeanza kutekelezwa, tunamwomba Mungu huu mradi ukamilike vizuri.”

Kulingana na wakazi wa eneo hilo, wakiwemo Marysiana na Jackson Magoto, wanaume na wanawake wamekuwa wakilazimika kuoga pamoja ziwani.

“Lakini mradi huu ukikamilika kila mmoja ataongea nyumbani kwa uhuru na faraga,” Magoto amesema.

Ofisa Mtendaji Kijiji cha Kwibara, Hassan Maximillian amesema mradi huo utawaepushia wananchi maradhi kama UTI na homa ya matumbo, kwani wamekuwa wakitumia maji yasiyo safi na salama kwa muda mrefu.

“Mradi huu utakuwa na chujio na maji yatawekewa dawa, hivyo tutapata maji safi na salama. Jukumu letu wananchi ni kuwa walinzi wa mradi huu maana ni mali yetu,” Maximillian amesema.

(Na Mwandishi wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages