NEWS

Tuesday 11 January 2022

Mbunge Kembaki akagua ujenzi wa madarasa na kusikiliza kero za machinga Tarime Mjini



MBUNGE wa Tarime Mjini, Michael Kembaki (mwenye suti) ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule za sekondari na msingi jimboni hapo, kutokana na fedha za kampeni ya kupambana na UVIKO-19.

Kembaki ametoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake ya kukagua miradi hiyo na mingineyo, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuelekeza fedha hizo kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya na maji.

“Mimi nina imani na Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, kwa sababu mwaka 2022 kwa mara ya kwanza wanafunzi wataingia shuleni na kuanza masomo kwa pamoja tofauti na miaka ya nyuma kulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa ilivyokuwa,” amesema.

Shule alizotembelea kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa ni pamoja na sekondari za Nyandoto, Nkongore, Nkende na shule ya msingi shikizi Taramoroni.

Pia, Mbunge Kembaki ametembelea mradi wa barabara ya Nyansurura - Kyore yenye urefu wa kilomita 1.50 ilioyo kwenye mpango wa kukarabatiwa, kisha amekagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano katani Ketare.



Kwa upande mwingine, Mbunge Kembaki amepata fursa ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Ndege katani Turwa na kusikiliza kero za wananchi, wakiwemo wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga).

Katika mkutano huo, Kembaki ameitaka Halmashauri ya Mji wa Tarime kuweka utaratibu mzuri wa kukusanya mapato katika soko la Rebu, bila kuathiri shuguli za wafanyabiashara hao.



Mbunge Kembaki ametoa agizo hilo baada ya wafanyabiashara hao kulalamikia adha ya kutozwa ushuru kila siku, tofauti na utaratibu wa siku za nyuma ambapo walikuwa wakilipa ushuru mara moja kwa wiki, yaani siku ya Jumapili.

Aidha, mbunge huyo amemtaka mkuu wa soko hilo na halmashauri hiyo kuwapanga machinga vizuri kwenye maeneo ya kuendeshea shughuli ili kuondoa malalamiko.

“Ninajua kero kubwa katika soko hili la Rebu ni changamoto ya wafanyabiashara wadogo wadogo, mkuu wa soko usiwasumbue wamachinga na michango isiyokuwa ya lazima,” Kembaki amesisitiza.

(Habari na picha zote: Geofrey John - Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages