MATOKEO ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba Mwaka 2021 yamedhihirisha ubora wa Shule ya Moregas English Medium (pichani juu), iliyopo eneo la Majengo Mapya katika mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime, Mara.
Shule hiyo ambayo awali ilijulikana kwa jina la Makima Englishi Medium, iling’ara katika matokeo hayo, chini ya uongozi wa mwekezaji mzawa, Cosmas Mseti aliyeipatia jina jipya la Moregas English Medium School baada ya kuinunua.
Moregas English Medium School ambayo ni shule ya kutwa na bweni, ilipata ufaulu wa juu na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya, ya pili kimkoa na ya 22 kitaifa katika matokeo hayo.
Ilivunja rekodi kwani watahiniwa wote 42 walipata ufaulu wa daraja A na wengi wao wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za bweni za vipaji maalumu katika mikoa mbalimbali nchini.
“Wanafunzi wetu 15 walichaguliwa kwenda kwenye shule za bweni za vipaji maalumu na kati ya hao, 10 ni wasichana,” Mkurugenzi wa shule hiyo, Mseti amesema katika mahojiano maalumu na Mara Online News, hivi karibuni.
Mkurugenzi Mseti akionesha sehemu ya miundombinu wezeshi ya shule hiyo.
Shule za vipaji maalumu walizochaguliwa kujiunga nazo ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Ufundi Chato iliyopo mkoani Geita, Songwe (Musoma, Mara), Tumaini (Singida) na Kilakala (Morogoro).
Nyingine ni Shule ya Sekondari ya Ufundi Mwadui (Shinyanga), Rugambwa Girls (Kagera), Mgugu (Morogoro), Balangdalalu (Manyara), Kilosa (Morogoro) na Bwiru Boys (Mwanza).
“Kati ya wanafunzi hao 42, watatu walipata A kwenye masomo yote na wote hao watatu ni wasichana,” anasema Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Emmanuel Edward.
Mkurugenzi Mseti anasema ndoto yake ni kuona Moregas English Medium School inakuwa shule bora kitaifa.
“Tunataka kuongoza kitaifa kwa kuwa shule bora kwa ufaulu, malezi na utoaji wa huduma,” anasema huku akijivunia miundombinu ya kisasa na walimu wa kutosha shuleni hapo.
Mseti anasema kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 612 wa darasa la awali hadi la saba na walimu 20, wakiwemo wa kike wanane.
Anasema ada za masomo katika shule hiyo ni nafuu na rafiki kwa Watanzania.
“Mfano wanafunzi wa kutwa kuanzia darasa la kwanza hadi la tatu wanalipa kila mmoja shilingi 340,000 kwa mwaka. Darasa la nne wote ni wa bweni kwa kuwa ni darasa la mtihani - kila mmoja analipa shilingi 1,010,000.
“Darasa la tano hadi sita wa kutwa wanalipa kila mmoja shilingi 400,000 na darasa la saba wote ni wa bweni kila mmoja analipa shilingi 1,200,000 kwa mwaka,” Mseti anafafanua.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kwa sasa Moregas English Medium School ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,000 na itaanza kufundisha somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa wanafujnzi mwaka huu.
“Wakati ninanunua shule hii ilikuwa na wanafunzi 36 lakini sasa tuna wanafunzi zaidi ya 600,” anasema huku akitaja ufundishaji wa viwango vya juu kama mojawapo ya sababu za ongezeko hilo.
Mseti ameendelea kuwekeza mamilioni ya fedha katika kuongeza na kuboresha miundombinu ya shule hiyo, kama vile mabweni na vyumba vya madarasa, likiwemo darasa la mafunzo ya kompyuta na TEHAMA.
Mkurugenzi Mseti akionesha jengo la mafunzo ya kompyuta na TEHAMA shuleni hapo.
Walimu wa shule hiyo wanataja baadhi ya ‘silaha’ zilizowezesha shule hiyo kung’ara kwenye matokeo ya mtihani wa taifa mwaka jana kuwa ni bidii na nidhamu kwa walimu na wanafunzi.
“Mungu kwanza, lakini tuna ushirikiano mzuri huku tukipata support kutoka kwa mkurugenzi wetu [Mseti], pia bidii na kujituma kwa walimu na wanafunzi.
“Tumedhamiria kuwa moja ya shule bora kitaifa. Mwaka huu (2022) ni kuongeza wastani wa ufaulu kutoka asilimia 267 hadi 288,” anasema Mwalimu Edward.
Mwalimu huyo anasema mazingira ya kupata elimu katika shule hiyo yameboreshwa.
“Wazazi walete watoto wao Moregas na tunaanza kufundisha somo la TEHAMA mwaka huu,” anasema.
One Day Yes ndio kaulimbiu (motto) ya Moregas English Medium School ambayo imejiwekea mikakati ya kuwa na walimu bora na wanafunzi wenye utayari kujifunza, usimamizi mzuri na mazingira rafiki.
“Ninaamini katika safari ya maisha, siku moja kila binadamu akifanya kazi kwa bidii anafikia ndoto zake,” Mkurugenzi Mseti anasema na kuendelea:
“Kaulimbiu ya One Day Yes inatokana na maneno niliyowahi kuandika kwenye baiskeli yangu, baadaye kwenye pikipiki na sasa kwenye shule hii kubwa yenye majengo ya kisasa na mazingira mazuri, ambayo inafaulisha wanafunzi kwenda shule za vibaji maalumu.”
Mkurugenzi huyo wa Moregas English Medium School anaweka wazi kuwa aliamua kubadilisha jina la shule hiyo kutoka Makima kuwa Moregas ili kuendana na ndoto yake ya kuifanya kuwa shule bora kitaifa.
“Niliamua kuwekeza kwenye sekta ya elimu baada ya kuona hakuna shule nzuri hapa na wazazi wengi walikuwa wanapeleka watoto kupata elimu nchi jirani,” anasema.
Anasema shule hiyo imeweka utaratibu unaowezesha wanafunzi kushiriki ibada kulingana na madhehebu yao katika mazingira ya shule.
“Shule yetu ina usafiri kwa wanafunzi wa kutwa na ninawakaribisha wazazi na walezi kuleta watoto Moregas,” Mseti anasema akihitimisha mahojiano hayo.
Uwekezaji huo wa Moregas English Medium School, pia umetengeza ajira za moja kwa moja na fursa mbalimbali kwa jamii inayoizunguka.
(Makala na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment