NEWS

Monday 17 January 2022

Sababu ya Mwenyekiti CCM Tarime kupenda kutalii Hifadhi ya Serengeti



MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho (pichani juu), ni kielelezo cha viongozi wa chama hicho tawala mkoani Mara, ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kwa mwaka 2021 pekee, Ngicho amefanya utalii wa ndani katika hifadhi hiyo bora Afrika zaidi ya mara tatu, huku akitumia magari yake yenye uwezo mkubwa kuzunguka hifadhini (game drive) kutazama wanyamapori.

“Mimi kwanza napenda sana wanyamapori, maana nilizaliwa ndani ya hifadhi - baba yangu akiwa mtumishi hifadhini,” Ngicho amesema katika mahojiano maalumu na Mara Online News ndani ya Hifadhi ya Serengeti, hivi karibuni.

Mapema mwaka huu, mwenyekiti huyo wa CCM pia alitembelea Hifadhi ya Serengeti kupitia lango la Lamai akiwa amefuatana na mke wake, Rhobi na Mkurugenzi wa Mara Online, Jacob Mugini na mke wake, Bhoke, ambapo walieleza kuvutiwa na wanyamapori wa aina nyingi, wakiwemo simba.


Simba wakipumuzika kivulini katika Hifadhi ya Serengeti

Aidha, Julai 2021, Ngicho aliungana na kundi la watalii wa ndani zaidi 60 kutembelea hifadhi hiyo katika safari iliyopewa jina la Mapokezi ya Nyumbu.


Kundi la watalii wa ndani wakipata maelezo kutoka kwa Mhifadhi Tutindaga George katika Hifadhi ya Serengeti.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele naye aliungana na watalii hao wa ndani katika safari hiyo, ambayo ilifungua utalii kupitia lango la Lamai lililopo kijiji cha Karakatonga.
Mwenyekiti Ngicho (kushoto) na DC Mntenjele wakifurahia utalii wa ndani katika Hifadhi ya Serengeti, hivi karibuni.

“Nawapongeza wabunifu wa jambo hili ambalo ni la kufurahia na la kifahari, isiwe mwanzo na mwisho na watalii hawa wawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Hifadhi ya Serengeti,” DC Mntenjele alisema.

Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii wa Hifadhi ya Serengeti, Tutindaga George alisema misafara wa nyumbu inayokuwa eneo la Kaskazini mwa hifadhi hiyo ni kivutio kikubwa kwa watalii.

“Watalii hawa wa ndani ‘wamepokea nyumbu’ katika eneo lao na sisi kama wahifadhi tumefarijika sana,” Mhifadhi Tutindaga alisema.

Misafara ya makundi ya nyumbu huongezeka katika eneo hilo la Kaskazini mwa Hifadhi ya Serengeti kwa takriban miezi minne - kuanzia Julai hadi Oktoba kila mwaka.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Kanda ya Magharibi, Neema Mollel alisema kundi hilo la watalii litakuwa chachu ya kuongezeka kwa watalii wa ndani katika Hifadhi Serengeti na nyingine nchini.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages