NEWS

Thursday 6 January 2022

Waitara ampiga kijembe Spika Ndugai akikagua ujenzi wa madarasa Tarime Vijijini



NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (pichani juu katikati) amelaani kauli ya Spika Job Ndugai ya kukosoa mikopo ya fedha kwa Tanzania.

“Haiwezekani tuko kwenye mtumbwi tunataka tuvuke na tuwavushe Watanzania, halafu mwenzetu anatoboa mtumbwi,” Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Vijijini amesema katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa jimboni, jana Januari 5, 2022.

Ameongeza “Nilikuwa na upungufu wa madarasa 116 katika jimbo langu la Tarime Vijijini, nikaletewa shilingi bilioni 2.4, nimepewa gari la kubeba wagonjwa, vituo vya afya vimejengwa, halafu anatokea mtu anapinga fedha za mkopo, huyo siyo mwenzetu.”

Mbunge Waitara (kushoto) akihutubia mkutano wa hadhara

Katika ziara hiyo, Mbunge Waitara amekagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule za sekondari Itiryo, Bwirege, Ganyange na Kangariani.

Ujenzi wa vyumba hivyo unagharimiwa na fedha za mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Waitara amewahimiza wananchi waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara ya Tarime Mjini - Nyamwaga - Serengeti kuondoka wenyewe ili kupisha upanduzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

"Lazima tuwambie wananchi ukweli, kama uko kwenye hifadhi ya barabara rudi nyuma mwenyewe, kwa sababu ujenzi kwa kiwango cha lami katika barabara ya Tarime - Serengeti umeanza," amesisitiza.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages