NEWS

Thursday 13 January 2022

Wakili Onyango avuta fomu ya uspika wa Bunge



WAKILI Otieno Onyango (pichani juu kushoto) amejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakili Onyango amechukua fomu hiyo katika ofisi ya CCM jijini Dodoma, leo Januari 13, 2022, ambapo baadaye katika mahojiano na wanahabari amesema yeye kama mwanasheria anastahili kuwa Spika wa Bunge hilo, kwani ni chombo kinachoendeshwa kisheria.

Wakili Otieno anasema alizaliwa mwaka 1980 mjini Tarime, Mara na alipata elimu ya msingi katika shule ya Turwa iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime.



“Nilisoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Ikizu iliyopo wilayani Bunda, kisha nikaenda kusoma kidato cha tano hadi cha sita katika Shule ya Sekondari ya Juu Makongo iliyopo jijini Dar es Salaam,” Wakili Onyango amesema na kuendelea:

“Baadaye nilikwenda kusoma shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Huddersfield nchini Uingereza kabla ya kwenda kusoma uzamili wa sheria katika Chuo Kikuu cha Derby nchini humo.

“Kisha nilirudi Tanzania na kwenda kusoma katika Shule ya Sheria kwa Vitendo (TSL) jijini Dar es Salaam - inayofundisha wanasheria kuwa mawakili.”

Wakili Onyango alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliowania kiti cha ubunge wa jimbo la Tarime Mjini katika uchaguzi mkuu mwaka 2020, ingawa kura za maoni hazikutosha kumwezesha kupeperusha bendera ya chama hicho tawala kwenye kinyang'anyiro hicho.

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages