NEWS

Saturday 26 February 2022

Polisi, TANAPA waendelea kutafuta watu ambao hawajaonekana baada ya gari kutumbukia mtoni hifadhini Serengeti



POLISI wanashirikiana na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutafuta watu watano ambao hawajaonekana baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia mtoni katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishabwamu, gari hilo aina ya Pickup lilipata ajali hiyo jana saa 4 usiku katika mto Warangi, wakati likitokea Fort Ikoma kuelekea Seronera ndani ya hifadhi hiyo.

“Juhudi za kuwatafuta zinaendelea na tunashirikiana na jeshi la polisi mkoa [wa Mara] na wilaya [ya Serengeti],” Mkuu wa hifadhi hiyo, Masana Mwishawa (pichani juu) ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu, jioni hii.

Mwishawa amesema ndugu wa watu hao nao wamefika eneo la tukio na kushuhudia utafutaji huo ukiendelea.

“Ndugu zao wamekujua tumeongea nao na tupo tunaendelea juhudi za kuwatafuta ndugu zao,” amesema.

Watu hao ni miongoni mwa 21 waliokuwa kwenye gari hilo wakati linatumbukia mtoni. Wengine 16 wakiwemo vibarua na watumishi wa TANAPA wameshaokolewa na kufanyiwa uchunguzi wa kiafya, kisha kuruhusiwa.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages