RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (pichani juu), anatarajiwa kuzuru mkoani Mara kushiriki maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM, kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 126.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma jana, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi amefafanua kuwa Rais Samia atawasili na kupokewa mkoani Februari 4, mwaka huu, kesho yake atashiriki sherehe za CCM kabla ya kutembelea miradi na kuzungumza na wananchi Februari 6 na 7 Musoma Mjini, Bunda, Musoma Vijiji na Butiama ambako pia atazuru katika kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
RC Hapi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma jana
RC Hapi ametaja miradi ya maji ambayo Rais Samia ataikagua na kuiwekea mawe ya msingi kuwa ni ule wa Mugango - Kiabakari (Butiama) na ujenzi wa chujio la maji (Bunda) itakayosambazia wananchi huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria.
Mingine ni maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa (Musoma) na ujenzi wa makao makuu ya wilaya ya Butiama.
#MaraOnlineNews-Updates
No comments:
Post a Comment