NEWS

Sunday 20 February 2022

RC Hapi: Sitaki kuona uchafu Sirari





MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi (pichani meza kuu katikati) ameagiza kuondolewa uchafu uliokithiri katika mitaa ya mji mdogo wa Sirari uliopo wilayani Tarime mpakanina nchi ya Kenya.

RC Hapi ametoa agizo hilo jana baada ya wananchi wa Sirari kulalamikia uwepo wa malundo ya uchafu katika maeneo wanayoishi na kufanya biashara, hivyo kumuomba kuingilia kati.

“Ukweli ni kwamba Sirari imejaa uchafu, kuna takataka nyingi na hii ni shida na kero ya kwanza,” mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Paul Jumanne amemueleza RC Hapi.

Wananchi hao wamekemea kero hiyo, akisema ni aibu kwa mamlaka husika kusimamia usafi katika eneo hilo la mpakani ambalo ni lango la kuingilia wageni wakiwemo watalii.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, RC Hapi ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) kushughulikia uondoaji wa uchafu huo haraka.

“Sitaki kuona uchafu Sirari, hili ni lango la kuingilia, wananchi wanalia uchafu,” mkuu huyo wa mkoa ameonya na kuagiza kazi hiyo ifanyike kuanzia leo Jumapili.

“Iwe mara ya mwisho, ni aibu RC kulalamikiwa uchafu, sitaki kusikia habari ya uchafu, kesho kazi ianze na nitafuatlia,” amesisitiza.

Aziagiza TRA, Uhamiaji
Katika hatua nyingine, RC Hapi amezitaka taasisi za serikali zilizopo mpakani Sirari, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji kuelimisha wafanyabiashara masuala yatakayoboresha shughuli zao katika eneo hilo, badala ya kuendelea kulaumiana.

Awali, baadhi wafanyabiashara wamezituhumu taasisi hizo mbele ya RC Hapi kwamba zimefanya mazingira ya biashara katika eneo hilo kuwa magumu, wakitolea mfano masharti magumu na matumizi ya nguvu kubwa kupambana na ‘bodaboda’ wanaovusha bidhaa kama vile saruji na nafaka mpakani hapo.

“Mazingira yetu ya kufanya biashara sio rafiki, sio kwamba hatutaki kulipa kodi ila tunaomba mazingira mazuri ili serikali ipate kodi na sisi tufanye biashara,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao, Laurent Nyabrangeti.

Akemea viongozi siasa, ubaguzi
Kwa upande mwingine, RC Hapi ametawaka viongozi wa kuchaguliwa na wananchi katika kata ya Sirari kuacha ubabe baada ya kulalamikiwa kutumia nguvu kutekeleza majukumu yao, hali inayochafua uhusiano baina yao.

“Uongozi ni dhamana, acheni ubabe usiokuwa na tija,” Mkuu wa Mkoa amesisitiza.

Pia, alikemea ubaguzi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wazawa katani Sirari dhidi ya Watanzania wengine kutoka nje ya kata hiyo, akisema kasumba hiyo haikubaliki. “Ruhusuni watu wawekeze, vijana wapate ajira,” amesema.

Wakati huo huo, RC Hapi ametangaza kumpatia Kamanda wa Wilaya ya Kipolisi Sirari, SSP Festo Ukulele zawadi ya Sh 500,000 baada ya wananchi kumpongeza kwa kazi nzuri ya kusimamia amani katika eneo hilo la mpakani.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages