NEWS

Monday 28 February 2022

Shule ya Moregas English Medium yaanzisha somo la kompyuta


KATIKA kuhakikisha Shule ya Msingi Moregas English Medium haibaki nyuma katika maendeleo ya teknolojia kuendana na dunia ya sasa, uongozi wa shule hiyo iliyopo Sirari wilayani Tarime, umeanzisha darasa maalum la kompyuta kwa wanafunzi wake wote.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Emmanuel Edward ameiambia Mara Online News shuleni hapo wiki iliyopita kwamba wameanzisha darasa hilo mwaka huu ili kuboresha ufundishaji na kuwezesha wanafunzi kuendana na ushindani wa kielimu duniani.

“Tumeanzisha darasa hili ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza masuala ya kidijitali mapema katika ngazi ya chini kabla hawajafikia elimu ya juu,” Mwalimu Edward amesema na kuongeza:

“Tunafanya haya kuisaidia serikali yetu ya Awamu ya Sita ambayo kwa sehemu kubwa inategemea matumizi ya intaneti, ambapo sasa wameanzisha anwani za makazi ikiwa ni mfumo unaotegemea pia intaneti na tunawafanya wanafunzi wetu waweze kuelewa masuala yote ya mawasiliano ya kidijitali.”


Wanafunzi wa Shule ya Moregas English Medium na mwalimu wao wakiendelea na somo la kompyuta darasani

Darasa hilo la kompyuta lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 48 kwa wakati mmoja, kila mwanafunzi akitumia kompyuta yake.

Mmoja wa wanafunzi wa shule ya Moregas English Medium amezungumzia darasa hilo akisema “Ninayo furaha sana kusoma somo la kompyuta, kwani linaniwezesha kujifunza vitu vingi kwa wakati mmoja na ninapata ujuzi sahihi.”

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, Rehema Yohana wa darasa la saba amesema “Ninapenda sana somo la kompyuta na hasa katika kipindi cha mazoezi ya kompyuta, ambapo ninaweza kujifunza mengi kwa njia ya video za katuni.”



Yapewa tuzo ya kitaifa
Hivi karibuni, Shule ya Moregas English Medium imetunukiwa Tuzo Maalumu kwa kuibuka mshindi wa kwanza kwa ufaulu mzuri wa somo la Kiingereza katika Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Darasa la Saba Mwaka 2021.

Tuzo hiyo imetolewa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, katika hafla maalumu iliyofanyika jijini Dodoma, wiki chache zilizopita.

Hafla nyingine ya kukabidhi tuzo hiyo ambayo ni kikombe maalumu cha ushindi, ilifanyika katika Hoteli ya Goldland mjini Tarime hivi karibuni, kwa kuhusisha Mkurugenzi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.


Mkurugenzi wa Shule ya Moregas English Medium, Cosmas Mseti (katikati waliokaa) akionesha tuzo ya kikombe waliyopewa na TAMISEMI, hivi karibuni. Wengine ni walimu na wanafunzi wa shule hiyo.

Mwalimu Emmanuel amesema ushindi huo ni zao la bidii ya walimu na wanafunzi katika kufundisha na kujifunza.

“Siri nyingine ya mafanikio haya ni ushirikiano wa dhati baina ya walimu, wazazi na wanafunzi,” ameongeza mwalimu huyo na kuahidi kutetea ushindi huo na kutwaa tuzo nyingine za makundi ya ufaulu mwaka huu.

“Huu ni mwanzo wa ushindi mkubwa tunaotarajia kuupata katika mtihani wa mwaka huu, ikiwemo kuingia kwenye kundi la tatu bora,” amesema Mwalimu Emmanuel.

Naye Mkurugenzi wa Shule ya Moregas English Medium, Cosmas Mseti ameungana na mwalimu huyo kuahidi ufaulu mzuri zaidi mwaka huu, huku akikaribisha wazazi kupeleka watoto kupata elimu bora katika shule hiyo.

“Tumefurahi kupata tuzo hii, tutazidi kuongeza bidii ili tuweze kufanya vizuri zaidi. Tunahamasisha wazazi kuleta watoto katika shule yetu, tuna walimu bora, lakini pia ada na mazingira ya kusoma ni rafiki,” Mkurugenzi Mseti amesema.

Ilivyong’ara matokeo
ya darasa la saba 2021
Mwaka jana, Shule yaa Moregas English Medium ilifunika majina ya shule zilizokuwa zikifanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la saba ndani ya halmashauri ya wilaya ya Tarime Mkoani Mara.

Shule hiyo ambayo hadi matokeo ya mwaka jana yanatangazwa ilikuwa ikijulikana kwa jina la Makima, ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya na nafasi ya pili kimkoa.

Watahiniwa wote 42 waliweka rekodi ya kupata ufaulu wa daraja la kwanza katika mtihani huo.

“Kati ya hao, wasichana watatu walipata A kwenye masomo yao yote,” amesema Mwalimu Emmanuel.

Aidha, shule hiyo iliongoza kwa kufaulisha wanafunzi waliochaguliwa kijiunga na sekondari za vipaji maalumu katika mikoa mbalimbali nchini.

Kitaifa ilishika nafasi ya 22 kwa shule zenye wanafunzi wa makundi makubwa (zaidi ya 40), ikiwa na wanafunzi 42 ambao walifaulu wote.

“Wanafunzi wetu 15 walichaguliwa kwenda sekondari za vipaji malumu za bweni, kati ya hao, 10 ni wasichana,” Mkurugenzi Mseti amefafanua.


Mkurugenzi Mseti katika mazingira ya shule yake ya Moregas English Medium

Ndoto ya mwekezaji huyo mzawa, ni kuifanya Moregas English Medium kuwa moja ya shule bora kitaifa.

“Tunataka kuongoza kitaifa kwa kuwa shule bora kwa ufaulu, walimu wa kutosha, malezi bora, miundombinu ya kisasa na huduma bora,” amesisitiza.

Shule ya Moregas English Medium ipo eneo la Majengo Mapya na kilometa 300 kutoka barabara kuu katika mji wa Sirari, mpakani na nchi ya Kenya.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages