
Na Mwandishi Wetu
Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA) Tanzania limewataka waumini wake kuwa watulivu na kuendelea kuamini kwamba taasisi hiyo ya kiroho inaendeshwa kwa kufuata sheria na taratibu.
Wito huo ulitolewa na uongozi wa SDA Tanzania jana Jumatano, Februari 25, 2026 kufuatia taarifa za vyombo vya habari kwamba Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo imevunjwa kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba Bodi ya Wadhamini inayodaiwa kuvunjwa bado inaendelea na utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi na taratibu za Kanisa tangu ilipoteuliwa Oktoba 12, 2023.
"Uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Union zote mbili bado upo, na unaendelea kusimamia misingi ya uwazi, uwajibikaji na uaminifu," taarifa hiyo ilieleza.
Iliongeza kuwa uongozi wa SDA unawahakikishia waumini wake kuwa taasisi yao iko imara na inaendeshwa kwa kufuatia sheria na taratibu.
Taarifa hiyo inafuatia habari zilizotangazwa/ kuchapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini zilizoeleza kuwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imevunja Bodi ya SDA Tanzania kwa tuhuma za matumizi mabaya madaraka na ubadhirifu wa mali za kanisa.
Taarifa ya SDA ililaani kutangazwa na kuchapishwa kwa habari hizo kutokana na kuegemea upande mmoja bila kuwahoji watuhumiwa.
"Uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato unasikitishwa na namna ya habari hiyo ilivyotolewa kwa kuegemea upande mmoja bila kuzingatia mizania ya taarifa kwa kusikiliza maelezo ya kanisa," taarifa hiyo ilisema.
No comments:
Post a Comment