NEWS

Wednesday 23 March 2022

AICT Mara na Ukerewe: Mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu boraKANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe (MUD) kwa kushirikiana na Taasisi ya Right to Play wamehimiza jamii kuzingatia suala la usawa wa elimu kwa watoto wa kike na kiume.

Afisa Mradi unaolenga kuongeza ubora wa elimu na elimu jumuishi, Rebeca Bugota (pichani juu) kutoka kanisa hilo ameyasema hayo wilayani Tarime, hivi karibuni.

Rebeca alikuwa akizungumza katika hafla ya kufunga michezo ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la nne kutoka shule za msingi Nyankoni na Itiryo.

“Lengo la mashindano haya ni kuihamasisha jamii ya hapa kuona umuhimu wa kuwapa elimu watoto wa kike, ndio maana tuko hapa tukishuhudia michezo mbalimbali kutoka kwa watoto hawa.

“Tunaendelea kuhamasisha umuhimu wa kuwapa watoto elimu, hasa kundi la watoto wa kike ambalo wakati mwingine wanasahaulika wakati na wao wana nafasi ya kupata fursa ya kusoma kwa ajili ya maisha ya baadaye,” Rebeca amesema.Naye mgeni rasmi wa bonanza hilo, Charles Mashauri ambaye ni Mratibu wa mradi huo mkoa wa Mara, amewataka wazazi na watu wote kuthamini elimu kwa mtoto wa kike.

“Tunapomuelimisha mtoto wa kike anakuwa chachu au kichocheo kwa maendeleo ya jamii, hivyo kwa pamoja tusichoke kuihamasisha jamii,” Mashauri amesisitiza.

Mashindano hayo yaliyobeba kaulimbiu inayosema “Muelimishe Msichana, kwa Maisha Bora ya Baadaye”, yamehusisha michezo tofauti, ikiwemo mpira wa miguu, riadha na mpira wa pete, huku washindi wakipewa zawadi mbalimbali.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

1 comment:

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages