NEWS

Friday 18 March 2022

Matokeo ya MOCK Kidato cha Sita 2022 Mkoa wa Mara hadharaniOFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Mara imetangaza matokeo ya Mtihani wa Utimilifu (Mock) kwa wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu, huku shule za Mkono na JK Nyerere zikiwa miongoni mwa tano bora.

Matokeo hayo yametangazwa na Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mara, Mwalimu Ahidi Sinene katika kikao kilichowashirikisha pia maofisa elimu wilaya na wakuu wa shule 26, kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma, leo.Sinene ametaja shule zilizoungana na Mkono na JK Nyerere katika kundi la tano bora, kuwa ni Songe, Natta na Chief Ihunyo.

Aidha, ametaja shule zilizoshika mkia katika mtihani huo kuwa ni Manga, Ikizu, Musoma Utalii, Musoma Ufundi na Nyamunga.

Shule nyingine za sekondari zilizofanya mtihani huo wa Mock mkoani hapa ni Bumangi, Tarime, Girango, Magoto, Bunda, Buturi, Mwembeni, Kasoma, Busegwe, Kibara, Serengeti, Borega, Ingwe, Mara, Makongoro na Nyanduga.


Sinene (kulia) na viongozi wengine wakifuatilia jambo kikaoni

Kwa mujibu wa Sinene, watahiniwa waliofanya mtihani huo katika shule zote 26 ni 2,543 (wavulana 1,612 na wasichana 931), huku wengine 46 (wavulana 35 na wasichana 11) hawakujitokeza kutokana na sababu mbalimbali.

“Mtihani huo ulifanyika Februari 21 hadi Machi 2, 2022 kwa lengo la kupima matayarisho ya wanafunzi hao kwa ajili ya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita utakaofanyika Juni mwaka huu,” amesema.

Mwalimu Sinene amefafanua kuwa waliofaulu mtihani huo kwa daraja la kwanza hadi la tatu ni 2,442 sawa na asilimia 96 ya wote walioufanya.Sinene ametaja masomo yaliyohusika na viwango vya ufaulu vikiwa kwenye mabano kuwa ni Baiolojia (3.4622), Historia (3.5875), Uchumi (3.5918), Kiingereza (3.7212), Uraia (3.7519), Kiswahili (3.9479), Jiografia (4.2732), Dini (4.3594), Kemia (4.3673), Hisabati (4.4497), Fizikia (4.8093) na Hesabu za Matumizi Msingi (5.1436).

Masomo ambayo wanafunzi walifanya vizuri, kwa mujibu wa Afisa Elimu Taaluma huyo wa mkoa, ni Uraia, Uchumi na Baiolojia.

Hata hivyo amesema “Matokeo haya hayaridhishi ukilinganisha na malengo ya mkoa na hata taifa. Tunahitaji kuongeza nguvu za pamoja kuhimiza ufundishaji na ujifunzaji, kufuatilia utekelezaji wa kalenda ya mtaala, ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo walimu na wanafunzi wasikate tamaa.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa (RAS) wa Mara, Dominicus Lusasi amewataka wakuu wa shule kusimamia vizuri walimu, kusikiliza na kutatua kero zao ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao kwa maendeleo ya wanafunzi.


Lusasi akizungumza kikaoni

“Natamani siku moja mkoa wa Mara uwe wa kwanza kitaifa, huo uwezo tunao,” Lusasi amesema.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Afisa Elimu Taaluma mwingine wa Mkoa wa Mara, Mwalimu Ayubu Mbilinyi, miongoni mwa viongozi wengine.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

1 comment:

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages