NEWS

Saturday 12 March 2022

Mbuge Chege ampongeza Waziri Jafo kwa kuunda Kamati Huru kuchunguza uchafuzi mto MaraWAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo ameunda Kamati Huru ya Kitaifa ya watu 11 kutoka sekta mbalimbali kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji na vifo vya samaki katika mto Mara.

Waziri Jafo ameunda kamati hiyo leo Machi 12, 2022 ikiwa ni siku moja baada ya Mbunge wa Rorya, Jafari Chege (pichani juu) kushauri iundwe kamati huru ya kuchunguza sakata hilo, baada ya Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt Samwel Gwamaka kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kamati imeundwa kwa kuwashirikisha wataalamu kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB).

"Iundwe kamati huru ambayo itatoa ukweli bila kuegemea upande wowote, hao watu wa NEMC na ofisi ya Bonde wanakuwepo kwemye maeneo hayo mara kwa mara, tunataka tume huru kufanya uchunguzi,” Chege alisema katika mazungumzo na Mara Online News kwa njia ya simu, jana.

Akizungumza na Mara Online News leo kwa njia ya simu, Mbunge Chege amempongeza Waziri Jafo kwa kufanyia kazi wazo lake hilo ili uchunguzi ufanyike kwa uhuru bila kupendelea upande wowote.

“Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Jafo, kwanza kufika lakini kubwa ni kukubali wazo langu la kuunda Kamati Huru ya kufanya uchunguzi wa suala hili la mto Mara kuwa na uchafu uliosababisha viumbe hai wakiwemo samaki kufa na kuongeza taharuki kwa wananchi wangu,” Chege mbunge wa Rorya na kuongeza:

“Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa siku saba na ameunda kamati independent (huru) itakayofanya kazi na kutoa taarifa, muhimu nashauri taarifa hiyo baada ya kukamilika iwe wazi na kila mbunge wa mkoa wa Mara ambaye mto huu unapita au unamwaga maji eneo lake la ziwani ashirikishwe na iwe wazi kwa wadau, wnaanchi na wabunge wa maeneo hayo ili kudhibiti na kuhakikisha hatua stahaki zinachukuliwa na kutojirudia na kama kuna madhara kwenye maji hayo basi wananchi watendewe haki kwa mujibu wa sheria za nchi.”

Mbunge huyo pia amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi wanayoendelea nayo ya kulinda maeneo yaliothirika na tukio hilo kuhakikisha wananchi hawaendelei kuyatumia ili kulinda afya zao.

“Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Maji naye afike na kuona namna ya kusaidia wananchi waliokumbwa na adha ya maji katika vijiji husika. Tumezuia wasitumie maji lakini lazima sasa Wizara ya Maji iendelee kuona mbadala wa maji kwa wnaanchi kwa maji yalio safi na salama,” Mbunge Chege amesema.

Siku chache zilizopita, katika baadhi ya maeneo ya mto Mara maji yalibadilika rangi kuwa meusi na samaki kuonekana wamekufa na kusababisha harufu kali ya uvundo, hali iliyozua taharuki kubwa kwa wananchi.

Uchimbaji wa madini unatajwa kuwa moja ya tishio la uhai wa mto Mara ambao ni muhimu kwa ustawi wa maisha ya maefu ya wananchi na ikolojia ya Serengeti.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages