NEWS

Thursday 10 March 2022

Mbunge Rorya ataka tume huru uchunguzi sakata la uchafuzi mto Mara, ashangaa ukimya wa Waziri JafoMBUNGE wa Rorya, Jafari Chege (pichani juu), ameikosoa tume iliyoundwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa mto Mara ambao umeua samaki na kusababisha harufu kali ya uvundo, akitaka iundwe tume huru kufanya uchunguzi huo.

"Iundwe tume huru ambayo itatoa ukweli bila kuegemea upande wowote, hao watu wa NEMC na ofisi ya Bonde wanakuwepo kwemye maeneo hayo mara kwa mara, tunataka tume huru kufanya uchunguzi,” Chege ameimbia Mara Online News leo asubuhi.

Aidha, Mbunge huyo kijana ameelezea kushangazwa na ukimya wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais (Muungano na Mazingira) tangu kutokea kwa tukio hilo ambalo limezua hofu na taharuku kwa maelfu ya wananchi katika vijiji vilivyo jirani na mto Mara.

“Waziri Jafo [Selemani Jafo] yuko kimya, ni wakati sasa kwa waziri huyu kijitokeza na kueleza umma wa Watanzania nini kinaenedelea mto Mara," amesema.

Katika hatua nyingine, Mbunge Chege amemuomba Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuangalia uwezekano wa kusaidia wananchi ambao wamezuiwa kutumia maji ya mto Mara kupata huduma ya maji hata kwa kuboresha visima vilivyopo.

"Leo ni siku ya tano, wananchi hawana huduma ya maji, Wizara ya Maji itoe fedha kugharimia uboreshaji wa visima vilivyopo na kuchimba vingine, maji ni uhai," Chege amesisitiza.

Jana jioni Mkurugenzi wa NEMC, Dkt Samuel Gwamaka akikaririwa na vyombo vya habari akisema tume imeundwa kuchunguza chanzo cha uchafuzi huo ambao haujawahi kushuhudiwa katika mto huo unaotiririsha maji Ziwa Victoria.

Uchimbaji wa madini unatajwa kuwa moja ya tishio la uhai wa mto Mara ambao ni muhimu kwa ustawi wa maisha ya maefu ya wananchi na ikolojia ya Serengeti.

(Imeandikwa na Mara Online News)

2 comments:

  1. Ni muhimu sana jambo hili lishughulikiwe haraka. Limezua taharuki kubwa.

    ReplyDelete
  2. Nampongeza sana Mbunge wangu, mtu makini, na mjasiri kwa hoja yake. IUNDWE TUME HURU, NC ISIHUSIKE!!
    Wao wataletewa taarifa ili wachukue hatua zingine, lakini kwenye uchunguzi wakae kando!!

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages