
Waziri Dkt. Rhimo Nyansaho
Na Mwandishi Wetu
Musoma
-------------
Wenyeviti wa halmashauri za mkoa wa Mara wameonesha furaha na imani yao kubwa kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya mkoa huo, wakisema ni kiongozi sahihi kwa nafasi hiyo nyeti.
Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kilichofanyika mjini Musoma jana Jumanne, Januari 6, 2026 kilimchagua Dkt. Nyansaho kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kupendekeza jina la Dkt. Nyansaho ambaye hakuwa kikaoni - kisha wajumbe wote wa Bodi wakaridhia kwa kauli moja.
Waziri Dkt. Nyansaho ni kati ya wabunge sita walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kisha kumteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Wakizungumza na Gazeti la Sauti ya Mara kwa nyakati tofauti baada ya uchaguzi huo, wenyeviti wa halmashauri mbalimbali mkoani Mara walimuelezea Dkt. Nyansaho kuwa ni kiongozi mchapa kazi na mpenda maendeleo wa kweli.
Waliongeza kuwa Dkt. Nyansaho ni kiongozi mwenye maono na bidii kubwa, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kusukuma utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii nzima.
“Tulimchagua Mhe. Nyansaho kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi wa Barabara kwa sababu ni kiongozi mchapa kazi na mpenda maendeleo wa kweli. Amefanya mambo mengi ya maendeleo katika mkoa wetu wa Mara,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Elias Ghati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Masalo Minza Shani, alisema wana matumaini makubwa kuwa kupitia nafasi hiyo, Dkt. Nyansaho atakuwa chachu ya mageuzi makubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara mkoani Mara.
“Tuna imani kubwa na Dkt. Nyansaho, hata kabla hajateuliwa kuwa Waziri, tumefanya naye kazi nyingi na hajawahi kutuangusha na tunampenda, ni kiongozi wa vitendo na mfano wa kuigwa,” alisema Masalo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma, alisema uchaguzi huo umeipa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kiongozi mwenye uwezo na ushawishi wa kusaidia kupatikana kwa utatuzi wa changamoto za miundombinu ya barabara katika mkoa huo.
“Kwanza Dkt. Nyansaho ni kipenzi cha wakazi wa mkoa wa Mara na mpenda maendeleo wa kweli, hivyo tumepata mtu sahihi ambaye tutashirikiana kutatua changamoto za barabara katika mkoa wetu,” alisema Makuruma.
Nao wabunge wa mkoani Mara walimpongeza Dkt. Nyansaho kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa na kuahidi kumpa ushirikiano unaohitajika.
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel, akizungumza katika kikao hicho aliahidi kwa niaba ya wabunge wa wenzake kwamba watakuwa tayari kumpa Dkt. Nyansaho ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake ndani ya Bodi hiyo.
Wakisisitiza zaidi, wenyeviti na wabunge hao walisema wana imani kubwa kuwa uongozi wa Dkt. Nyansaho katika Bodi hiyo utaongeza kasi ya maendeleo na kuimarisha mtandao wa barabara kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa mkoa wa Mara.
No comments:
Post a Comment