WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Butiama mkoani Mara, inatarajia kuongeza kiwango cha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa wilaya hiyo, kutoka asilimia 63 ya sasa hadi 70, kufikia Juni mwaka huu.
Hatua hiyo itatokana na kukamilika kwa miradi saba ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4 zilizotolewa na Serikali kugharimia utekelezaji wa miradi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022, chini ya usimamizi wa RUWASA.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Butiama, Mhandisi Mafuru Dominico ameyasema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, waliotembelea baadhi ya miradi hiyo, jana.
Moja ya miradi iliyotembelewa ni wa kijiji cha Biatika unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 663, kwa kuhusisha uchimbaji mtaro na ulazaji mabomba ya maji kwa urefu wa kilomita 19.
Utandazaji mambomba ikiendelea katika mradi wa maji Biatika
“Mradi huu una vituo 25 vya kuchotea maji na tayari tenki lake lenye uwezo wa kuchukua lita 135,000 za maji (kwa wakati mmoja) limeshajengwa,” amesema Mhandisi Dominico.
Kwa mujibu wa meneja huyo, mradi huo pia umeshajengewa vyanzo viwili na utawezesha wakazi 6,723 wa vijiji vya Biatika na Kinyariri kupata huduma ya maji safi na salama.
Mhandisi Mafuru Dominico akifafanua jambo katika mahojiano na waandishi wa habari (hawapo pichani) kijijini Masurura.
Amesema kwa sasa wanavijiji hao wanalazimika kutumia maji ya visima vya asili yasiyo salama, huku mifugo yao ikinyweshwa kwenye mabwawa.
Waandishi wa habari pia wametembelea mradi wa maji kijijini Masurura unaokarabatiwa kwa gharama ya shilingi milioni 150.
Sehemu ya miundombinu ya mradi wa maji kijijini Masurura
Mhandisi Dominico amesema mradi huo una uwezo wa kuhudumia watu 4,030 na kwamba tayari kaya 26 zimeunganishiwa huduma ya maji safi na salama ya bomba majumbani.
“Mradi huu wa Masurura una tenki la lita 100,000, vituo 20 vya kutolea maji na chanzo chake ni kisima kirefu,” amebainisha.
Viongozi na wakazi wa maeneo ya miradi hiyo wameishukuru RUWASA, Wizara ya Maji chini ya Waziri Jumaa Aweso na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapelekea miradi ya huduma ya maji safi na salama.
“RUWASA imekuwa suluhisho la uhaba wa maji kwa wananchi wengi Butiama,” Mkuu wa Wilaya (DC) ya Butiama, Moses Kaegele amewambia waandishi wa habari.
DC Kaegele akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment