NEWS

Saturday, 12 March 2022

Vifo vya samaki mto Mara: Mafuta, grisi vyatajwa



BODI ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imetaja chanzo cha uchafuzi wa maji na vifo vya samaki katika mto Mara eneo la Kirumi darajani.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Bodi hiyo kwa vyombo vya habari leo Machi 12, 2022, hali hiyo imesababishwa na kiwango kikubwa cha mafuta na grisi kuliko kinachotakiwa kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania.

Sababu nyingine kwa mujibu wa taarifa hiyo ya LVBWB, ni kukosekana kwa hewa ya oksijeni kwenye maji (DO), kuliko kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania.

Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mkurugenzi wa LVBWB, Renatus Shinhu, imetaja vijiji vilivyoathirika na uchafuzi huo kuwa ni pamoja na Kirumi, Kwibuse, Marasibora na Ryamisanga.

LVBWB imetoa ufafanuzi huo baada ya kufika eneo la tukio Machi 8, 2022 na kuchukua sampuli za maji kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.

“Kiwango kikubwa cha mafuta kwenye maji ndicho kilichosababisha kuisha kwa hewa ya oksijeni kwenye maji na kuathiri viumbe hai ikiwa ni pamoja na samaki.

“Kuhusu rangi ya maji, uchunguzi wa kimaabara unaendelea ili kubaini kilichosababisha maji haya kuwa meusi,” imeeleza taarifa hiyo ya LVBWB na kuongeza:

“Kwa mujibu wa majibu ya maabara ya tarehe 11/03/2022, kiwango cha hewa ya oksijeni kwenye maji kinaongezeka na kiwango cha mafuta kinapungua.”

Hata hivyo, Bodi hiyo haikutaja chanzo cha mafuta na grisi vilivyofyonza hewa ya oksijeni, kuchafua maji na kuua samaki katika mto Mara ni kipi.

Taarifa hiyo ya LVBWB imekuja saa chache baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo kutembelea eneo la tukio leo na kuunda Kamati Huru ya Kitaifa ya watu 11 na kuipa muda wa siku saba kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji na vifo vya samaki katika mto Mara.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages