NEWS

Tuesday 8 March 2022

RUWASA Tarime yatengewa Sh bilioni 4.3 kugharimia utekelezaji miradi ya maji



Tenki la mradi wa maji Sirari

KATIKA jitihada za kuboresha huduma ya maji safi na salama wilayani Tarime, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi kadhaa yenye thamani ya shilingi bilioni 4.3.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Malando Masheku amewambia waandishi wa habari waliotembelea baadhi ya miradi hiyo leo Machi 8, 2022 kwamba utekelezaji unaendelea chini ya programu za CSR, P4R, PBR, UVICO-19 na Mfuko wa Maji wa Taifa.


Mhandisi Masheku

Mhandisi Masheku ametaja miradi inayoendelea kutekelezwa mwaka huu wa fedha na thamani zake kwa viwango vya milioni zikiwa kwenye mabano kuwa ni Matongo - Nyangoto (998), Sabasaba (500), Itiryo (498), Kitawasi – Masurura - Masanga (389), Mtana (349), Gimenya (184) na Wegita (33).

Waandishi wa habari wameshuhudia baadhi ya miradi hiyo utekelezaji ukiendelea kwa hatua mbalimbali.

Baadhi ya miradi iliyokwisha kukamilika kwa awamu ya kwanza na kuendelea kutoa huduma ya maji safi na salama ni Sirari na Gamasara.


Wanawake wakichota maji ya mradi wa Sirari

Mradi wa Sirari uliogharimu shilingi milioni 534 umejengewa tenki la kisasa la lita 100,000 na mashine ya kusukuma maji kwa umeme kutoka visima vya asili.

Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Sirari, Amos Sagara, mradi huo unahudumia wakazi zaidi ya 60,000 wa kata hiyo na kata jirani za Gwitiryo na Regicheri.


Diwani Sagara akionesha kisima cha asili ambacho ni chanzo cha mradi wa maji Sirari

Wakazi wa mji wa Sirari, Sarah Yakobo, Pendo Deus na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani City wameungana na Diwani Sagara kuipongeza RUWASA na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea mradi huo.

Kwa upande wa mradi wa Gamasara, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji, Rahel Onyango na Diwani wa eneo hilo, Fred Sabega wameomba Serikali kupitia RUWASA iendelee kupanua mradi huo uweze kuhudumia watu zaidi ya 7,000 wanaonufaika nao kwa sasa.


“Tunauzia wananchi maji kwa bei ya shilingi 50 kwa ndoo moja ya lita 20, ambapo wastani wa mapato tunayokusanya kwa mwezi ni laki sita msimu wa kiangazi na 250,000 wakati wa masika,” Katibu wa mradi huo, Paulo Juvenalis amesema.

Kwenye mradi wa Magoto, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles, mbali na kumshukuru Meneja wa RUWASA, Mhandisi Masheku kwa kusimamia vizuri utekelezaji wake, wameomba maji yake yatibiwe na ujengewe uzio kuuimarishia usalama.

Mwenyekiti Kiles (kulia) akizungumza na waandishi wa habari. Kushoto ni Mbunge Waitara

Aidha, Mwenyekiti Kiles ameihimiza RUWASA kuhakikisha inashirikisha viongozi na wananchi wa eneo husika katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Mhandisi Masheku amesema kwa sasa mahitaji ni lita milioni 11.9, wakati upatikanaji ni lita 8.33 (sawa na asilimia 70 ya mahitaji) kwa siku.

Katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Meneja huyo wa RUWASA amesema mahitaji ya maji ni lita milioni sita, huku yanayopatikana ni lita milioni 1.5 (sawa na asilimia 45 ya mahitaji) kwa siku.

Amesema ofisi yake imeomba serikalini shilingi milioni 410 kwa ajili ya kugharimia uboreshaji wa chujio la maji ya chanzo cha Nyanduruma ili kuwezesha wakazi wa mji wa Tarime kupata maji safi, tofauti na sasa ambapo ni ya rangi ya vumbi.

Ujenzi tenki la maji la mradi wa Itiryo unaendelea

Mhandisi Masheku ametaja changamoto kubwa inayoikabili ofisi yake kwa sasa kuwa ni kiu ya kupata gari kwa ajili ya kurahisisha na kuimarisha safari za ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi ya maji wilayani.

Hata hivyo, Mhandisi Masheku aliwashukuru na kuwapongeza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Rais Samia kwa kuendelea kuipatia wilaya ya Tarime fedha za kutekeleza miradi ya kuwaboreshea wananchi huduma ya maji safi na salama.

“Tunampongeza sana Waziri wetu wa Maji, Aweso na Rais wetu mama Samia. Kaulimbiu yetu katika wilaya ya Tarime ni: Palipo na watu lazima maji yafike, tunatekeleza kwa vitendo,” amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele ameungana na Katibu wa CCM Wilaya, Valentine Maganga, Mbunge Waitara, Mwenyekiti wa Halmashauri, Kiles na Mhandisi Masheku kusisitiza kuwa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji ya kutosheleza mahitaji ya wakazi wa wilaya hiyo ni mradi tarajiwa wa kutoa maji Ziwa Victoria.


DC Mntejela akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake


Katibu Maganga akisisitiza jambo katika kikao na waandishi wa habari ofisini kwake

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages