NEWS

Monday 7 March 2022

RUWASA yawaondolea wanakijiji Rorya adha ya kufuata maji Kenya



KAYA zaidi ya 400 katika kijiji cha Ng’ope wilayani Rorya, Mara zimeondokana na adha ya kufuata maji nchini Kenya, baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwajengea mradi wa maji safi na salama.

“Tunaishukuru sana Serikali kupitia RUWASA kutujengea mradi huu, kwa muda mrefu tulikuwa tukilazimika kutembea umbali wa kilomita sita kwenda kutafuta maji kule Olasi, Kenya,” Magreth Odira aliwambia waandishi wa habari waliotembelea mradi huo jana.


Magreth akizungumza na waandishi wa habari

Magreth ambaye amekabidhiwa dhamana ya kuuza maji ya mradi huo kwa bei ya shilingi 50 kwa ndoo ya lita 20, alisema wanakijiji wengi kwa sasa wamefarijika kusogezewa huduma hiyo karibu na kwa bei nafuu.

“Kule Olasi tulikuwa tukiuziwa ndoo moja kwa shilingi 25 za Kenya (sawa na shilingi 500 za Tanzania), kama hauna hela unapewa kazi ya kusomba tope ndoo tatu hadi nne kutoka bwawani, ndipo unaruhusiwa kuchota maji,” Magreth alieleza.

Naye Mwenyekiti wa Mradi wa Maji Ng’ope, Zakayo Tito alisema wanakijiji wameanza kunufaika na mradi huo Februari mwaka huu.

“Tunauona mradi huu wa maji safi na salama kama dhahabu, ni baraka kubwa. Tunaishukuru sana RUWASA na Serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan,” Tito alisema.


Tito (kulia) akiwa kwenye kioski cha kuuza maji kijijini Ng'ope

Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rorya, Mhandisi James Kishinhi, utekelezaji wa mradi huo ulihusisha uchimbaji kisima, ujenzi wa kioski na ununuzi wa tenki lenye mita za ujazo 10,000.

“Lengo la mradi huu ni kuwaondolea wakazi wa kijiji hiki cha Ng’ope usumbufu wa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji nchini Kenya,” Mhandisi Kishinhi alisema na kuweka wazi kuwa RUWASA ilitumia shilingi milioni 198 kugharimia utekelezaji wake.


Mhandisi Kishinhi

Meneja huyo aliongeza kuwa bado wana mpango wa kupanua mradi huo kwa kutumia chanzo cha Ziwa Victoria kuwezesha wakazi wa kijiji cha Ng’ope zaidi ya 13,000 kupata maji ya kutosheleza mahitaji yao.

Kwa upande mwingine, waandishi wa habari walitembelea mradi wa maji unaoendelea kuboreshwa na RUWASA katika kijiji cha Gabimori, Rorya.

Tenki la maji kijijini Gabimori

Diwani wa Kata ya Kyangasaga, alisema kijiji hicho kinaundwa na kaya 521 zenye watu zaidi ya 18,000 na kwamba wengi wao wanatarajiwa kuanza kupata huduma ya maji safi na salama baada ya RUWASA kukamilisha utekelezaji unaokusudiwa.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages