NEWS

Friday 11 March 2022

Serikali yaitengea RUWASA Sh bilioni 5.6 kugharimia utekelezaji miradi ya maji Bunda



UPATIKANAJI wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wilayani Bunda, unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 60 ya sasa hadi 67, baada ya miradi 15 inayoendelea kutekelezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilika.

Utekelezaji wa miradi hiyo, kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bunda, Mhandisi William Boniphace, umetengewa shilingi bilioni 5.6 kutoka serikalini kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

“Miradi iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, kufikia Juni mwaka huu yote itakuwa imekamilika,” Mhandisi Boniphace amewambia waandishi wa habari waliotembelea baadhi ya miradi hiyo, jana.


Mhandisi Boniphace akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

Mhandisi Boniphace amesema kati ya wakazi 378,000 wa wilaya ya Bunda, wanaopata huduma ya maji safi na salama kwa sasa ni 263,000, waliobaki wanatumia ya mabwawa, mito na visima vya asili - yasio salama.

Waandishi wa habari wamefika katika mradi wa maji wa kijiji cha Karukekere unaohudumia watu 13,000 katika kijiji hicho na vijiji jirani vya Kabainja, Chingurubira na Kenkombya.

Kwa mujibu wa Mhandisi Boniphace, mradi huo umegharimu shilingi milioni 724.7.

Mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji ya mradi huo, Robert Masaga amefafanua kuwa wananchi hao ni pamoja na wateja 82 waliounganishiwa huduma ya maji ya bomba katika miji yao.


Mojawapo ya kituo cha kuchotea maji cha mradi wa Karukekere

Masaga ameishukuru RUWASA kwa kutembelea kijijini hapo mara kwa mara na kuelimisha wajumbe wa kamati ya mradi huo majukumu yao na namna nzuri ya kusimamia fedha za mauzo ya maji.

“Lakini pamoja na hayo, tunaomba Serikali ituunganishie umeme kwa ajili ya kusukuma maji kutoka kwenye vyanzo vya mradi wetu wa Karukekere, ili tuondokane na matumizi ya dizeli kwa gharama kubwa,” amesema.

Miradi mingine ya maji inayotekelezwa mwaka huu chini ya usimamizi wa RUWASA katika wilaya ya Bunda, iliyotembelewa na waandishi wa habari ni Kibara na Bitaraguru.

Meneja wa RUWASA Bunda, Mhandisi Boniphace, amesema mradi wa Kibara wenye uwezo wa kuhudumia watu 21,000 umetengewa shilingi milioni 558 na Bitaraguru utakaohudumia watu 7,200 baada ya kukamilika - bajeti yake ni shilingi milioni 500.


Tenki la maji la mradi wa Kibara

Mhandisi Boniphace ametaja kikwazo kikubwa katika miradi ya maji inayosimamiwa na RUWASA wilayani Bunda kuwa ni uharibifu wa miundombinu, ukiwemo ukataji wa mabomba ya maji.

“Tunaendelea kuelimisha wananchi umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya miradi ya maji,” Mhandisi Boniphace amesema, huku akiishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuelekeza fedha nyingi wilayani Bunda kugharimia utekelezaji miradi ya kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages