NEWS

Tuesday 19 April 2022

Mbunge Waitara ahutubia wananchi akinyeshewa mvua jirani na mgodi wa North MaraMBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (pichani juu mwenye suti nyeusi), jana jioni alihutubia wananchi huku akinyeshewa mvua katika kijiji cha Kewanja jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Aliwashangaza wengi pale alipowakatalia wasaidizi wake kumkinga na mwavuli asinyeshewe na alitumia saa zaidi ya moja kuhutubia wananchi, baadhi yao wakiwa wamejikinga chini ya miti na wengine kwenye kuta za nyumba.

Katika mkutano huo, Mbunge Waitara alianza kwa kusikiliza kero za wananchi kupitia kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho na madiwani wa kata za Kewanja, Matongo na Nyamwaga.


Mbunge Waitara akisalimia watoto alipowasili eneo la mkutano huo.

Hotuba yake iliangazia miradi ya kijamii inayohitaji uboreshaji na suala la malipo ya fidia kwa wananchi wanaohamishwa kupisha shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa North Mara.

Alitumia nafasi hiyo pia kukiomba chama tawala - CCM wilayani Tarime kusaidia kuishawishi Serikali mkoani Mara iruhusu shilingi bilioni 11.244 za Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zitolewe na mgodi huo ili zitumike kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Kuhusu malipo ya fidia kwa wanavijiji wanaopisha mgodi wa North Mara, Mbunge Waitara aliahidi kuendelea kufikisha malalamiko yaliyopo kwa mamlaka husika kwa hatua za ufumbuzi.


Kabla ya kuhutubia mkutano huo, Mbunge Waitara ambaye alifuatana na Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Valentine Maganga, alikagua miundombinu ya mradi wa maji wa Nyangoto katika kata ya Matongo, wenye thamani ya shilingi milioni 998 - ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 30.

Habari ya kina kuhusu kero za wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi huo zilizowasilishwa kwa Mbunge Waitara, zitachapishwa kwenye toleo lijalo la gazeti la Sauti ya Mara.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages