NEWS

Wednesday 20 April 2022

Serikali Mkoa wa Mara yamkataa Meneja Uhusiano wa Barrick North Mara, yaagiza yeye na wenzake wa CDC wachunguzwe


MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi (pichani), amesema Serikali ya mkoa huo haiko tayari kufanya kazi na Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.

Aidha, RC Hapi ametangaza kuivunja Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) iliyokuwa inapanga matumizi ya miradi ya kijamii kutokana na fedha za Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zinazotolewa na mgodi huo katika vijiji 11 vinavyouzunguka.

Sambamba na hayo, mkuu huyo wa mkoa ameviagiza vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwafungulia majalada ya uchunguzi viongozi wa CDC.

RC Hapi ametoa matamko hayo kwenye kikao cha wadau wa maendeleo ya kisekta mkoani Mara, kilichofanyika mjini Musoma, leo Aprili 20, 2022.

"GM [akimaanisha Meneja Mkuu wa mgodi huo] fanya mabadiliko ya Meneja Uhusiano, hatuko tayari kufanya kazi naye..." amesisitiza RC Hapi.

Ameweka wazi sababu ya kumkataa meneja huo kuwa ni kutokana na kuhusika kwake katika matumizi mabaya ya fedha za CSR kupitia CDC ambayo haina 'miguu ya kisheria'.

Amedai kuwa CDC imekuwa ikipanga matumizi ya miradi ya kijamii inayogharimiwa na fedha za SCR bila kuwashirikisha wataalamu husika wala wananchi walengwa.

"CDC inaamua hadi miradi ya maji, barabara, afya na elimu, ina wataalamu gani?" amehoji RC Hapi.

Awali, kabla ya matamko na maelekezo hayo, Kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Robert Gabriel (aliyehamishiwa mkoani Mwanza), iliwasilisha kwa RC Hapi ripoti iliyobaini uwepo wa matumizi mabaya ya shilingi bilioni tano za CSR zilizotolewa na mgodi wa North Mara kwa ajili ya kugharimia miradi ya kijamii katika vijiji 11 vinavyouzunguka ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Fedha hizo zilitolewa na kuanza kutumika mwaka 2020 wakati halmashauri hiyo na jimbo la Tarime Vijijini vikiongozwa na madiwani na mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho, Mbunge wa Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara, amempongeza RC Hapi kwa kuvunja CDC hiyo, kwani hata yeye amemekuwa akikemea wizi wa fedha za CSR.

Hata hivyo, Waitara ametumia nafasi hiyo pia kumshauri mkuu huyo wa mkoa kuitisha kikao na madiwani na wananchi wa Tarime Vijijini ili kuwaeleza maamuzi na maelekezo hayo ya kiserikali.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages