
Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kilichofanyika mjini Musoma jana na kuikataa bajeti ya barabara ya Hifadhi ya Taifa Serengeti
Musoma
------------------
Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara imekataa kupitisha makadirio ya bajeti ya barabara za Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA) - kiasi cha shilingi bilioni 3.189 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kutokana na kutoakisi mahitaji halisi ya matengenezo ya barabara hizo.
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alitangaza msimamo wa kuikataa bajeti hiyo, na kuungwa mkono na wajumbe karibu wote wa kikao cha Bodi hiyo kilichofanyika mjini Musoma, Machi 2, 2026.
“Nina wasiwasi sana… kama bajeti yenyewe mnayotenga ni bilioni tatu wakati lile daraja moja tu la kiboko linakula hiyo bilioni tatu mtatusaidia kweli kwa eneo lote?” alihoji RC Mtambi na kuendelea:
“Kwa hiyo, sisi tunaikataa hiyo bajeti, kama Road Board ya Mkoa tunakurudishia hiyo bajeti siyo realist (halisi) ya miradi inayohitajiwa.”
Hivyo, RC Mtambi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho cha Bodi ya Barabara aliishauri SENAPA kuongeza bajeti itakayotosha kugharimia maboresho yanayohitajika kwenye barabara za hifadhi hiyo.
“Tunaomba mje na bajeti inayofanana na changamoto iliyopo, bilioni tatu hapana, hiyo hailingani kabisa, lakini tumefurahi kwamba na ninyi mmeiona kwamba haitoshi, sasa kama haitoshi sisi hatuwezi kuipokea hapa.
“Sisi ambao tumepewa dhamana na serikali - ya kusimamia miundombinu katika maeneo haya, tukilikubali hili tutaonekana na sisi si watendaji wazuri,” alisisitiza RC Mtambi.
Kiongozi huyo wa mkoa alihitimisha hoja hiyo kwa kuwauliza wajumbe wa kikao hicho: “Wajumbe, niwaulize mmeikubali au tumrudishie bajeti yake?” Idadi kubwa ya wajumbe walijibu: “Hatuikubali.”
Wajumbe wa kikao hicho waliounga mkono hoja ya kuikataa bajeti hiyo ya SENAPA ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, ambaye naye alishangaa kuona hifadhi ambayo imekuwa ikishinda tuzo za kimataifa ikiwasilisha bajeti finyu ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
“Naunga mkono kwamba hii bajeti tuikatae... hizo clips za gari limepelekwa na maji, watu wamekwama katika hifadhi ambayo tuna tuzo nyingi za kimataifa - hili jambo halikubaliki. Warudi nayo wakaandae bajeti inayotosha ili tupitishe wafanye marekebisho ya barabara za hifadhi yetu ya Serengeti,” alisema Waitara.
Awali, akiwasilisha makadirio ya bajeti hiyo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Ismail Omari, alisema wamepanga kutumia shilingi 3,189,500,003 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kugharimia matengenezo ya barabara, vivuko na viwanja vya ndege ndani ya hifadhi hiyo ambayo eneo lake kubwa lipo mkoani Mara.
Hata hivyo, Mhifadhi Ismail alidokeza kwamba kutokana na uharibifu mkubwa wa barabara uliosababishwa na mvua, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linaangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya SENAPA ili nayo pia iweze kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara zake.
Katika kikao hicho, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 iliomba kuidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 20.6, huku Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa ikiomba kuidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 47.676 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Meya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri, wadau wa barabara, wakuu wa baadhi ya taasisi za umma na maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
No comments:
Post a Comment