NEWS

Friday 8 April 2022

Vijiji vya pembezoni Musoma Vijijini vyapata maji ya bomba kutokana na fedha za UVIKO-19

Profesa Sospeter Muhongo

MAMILIONI ya fedha yaliyotolewa na Serikali chini ya mpango wa kupambana na UVIKO-19, yameendelea kugharimia utekelezaji wa miradi ya kusambaza maji ya bomba kwenye vijiji mbalimbali katika jimbo la Musoma Vijijini.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini jana, chanzo cha miradi hiyo ya maji ni Ziwa Victoria.

Miongoni mwa fedha hizo ni shilingi milioni 300 zilizoelekezwa kwenye mradi wa kusambaza maji ya bomba katika vijiji vya Nyasaungu katani Ifulifu na Kurwaki (Mugango).

Nyingine ni shilingi milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya kugharimia mradi wa usambazaji maji ya bomba kwenye vijiji vya Kanderema, Bugoji na Kaburabura katani Bugoji.

Aidha, Serikali imeongeza shilingi zaidi ya milioni 400 kugharimia mradi huo kutokana na vijiji hivyo kuwa mbali na Ziwa Victoria, ambapo sasa kata yote ya Bugoji itapata huduma ya maji safi ya bomba.

“Wakazi na viongozi wa vijiji hivyo, kata ya Bugoji na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwatatulia tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji ya bomba,” imesema taarifa hiyo.

Vijiji vyote 68 vinavyounda jimbo la Musoma Vijijini vina miradi mbalimbali ya kusambaziwa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria, kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka ofisi ya Mbunge Muhongo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages