
Zao la bangi shambani
Na Mwandishi Wetu
Mara
--------------
Mkoa wa Mara unaendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya kilimo cha bangi, huku Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikitangaza kuwa uzalishaji wa zao hilo haramu umepungua kwa takriban asilimia 80 kufuatia operesheni endelevu zinazotekelezwa na serikali.
Mafanikio hayo yanatajwa kuwa ishara ya kuimarika kwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ambapo wananchi wa maeneo ya mkoa huo yaliyokuwa yamekithiri kwa kilimo cha bangi, hususan wilaya ya Tarime, wamebadilika na kujielekeza kwenye shughuli halali za uzalishaji.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amethibitisha kuwa kilimo cha bangi katika mkoa wa Mara kimepungua kwa takriban asilimia 80 kutokana na operesheni endelevu zinazotekelezwa na serikali katika kukabiliana na uzalishaji wa dawa za kulevya.
Akizungumza wiki iliyopita, baada ya kuhitimisha operesheni maalum zilizofanyika katika wilaya za Tarime na Rorya, Lyimo alisema operesheni hizo zimefanikisha kuteketezwa kwa mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 291.2, kukamatwa kwa magunia 15 ya bangi kavu na pikipiki nne zilizokuwa zikitumika katika shughuli hizo haramu.
Aidha, watu wawili wamekamatwa huku uchunguzi ukiendelea kuwabaini na kuwakamata washirika wengine waliohusika katika mtandao huo.
Alisema mafanikio hayo yanathibitisha ufanisi wa operesheni za serikali, akibainisha kuwa mwaka 2024 ekari zaidi ya 3,500 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika mkoa wa Mara.
Hatua hiyo, alisema imechangia kwa kiwango kikubwa kupunguza uzalishaji wa bangi na kudhoofisha mtandao wa kilimo hicho katika maeneo yaliyokuwa yakiathirika zaidi.
"Matokeo haya yanaonesha kuwa juhudi za serikali zinaendelea kuzaa matunda. Wananchi wengi wameanza kuachana na kilimo cha bangi na kuelekeza nguvu zao katika shughuli halali za uzalishaji zinazowanufaisha wao, familia zao na taifa kwa ujumla," alisema Lyimo.
Hata hivyo, Kamishna Jenerali huyo aliwataka wananchi ambao bado wanajihusisha na kilimo cha bangi kuachana na shughuli hiyo mara moja na kuwekeza katika kilimo halali cha mazao ya chakula na biashara.
Aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na DCEA na vyombo vingine vya dola kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na uzalishaji, usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.
Alisisitiza kuwa DCEA itaendelea kuimarisha operesheni, doria na uchunguzi wa kina katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na makosa ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake Afisa Tarafa ya Inchage, Stephano Peter Kiabaroti, alisema uwekezaji unaoendelea kufanywa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeongeza uwezo wa DCEA kutekeleza operesheni zenye matokeo makubwa katika kudhibiti na kutokomeza kilimo cha bangi.
Alisema wananchi wengi waliokuwa wakitegemea kilimo hicho sasa wamehamia katika uzalishaji halali wa mazao ya chakula na biashara na shughuli za ufugaji, hatua ambayo imeanza kuleta manufaa ya kiuchumi kwa familia na jamii kwa ujumla.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Rozana, Kurwa Robert, alisema kabla ya operesheni hizo matumizi na biashara ya bangi vilichochea ongezeko la vitendo vya uhalifu, huku baadhi ya vijana wakijihusisha na makundi ya uhalifu na kujichukulia sheria mkononi.
Alisema baada ya DCEA kuimarisha operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi, hali ya usalama imeimarika kwa kiasi kikubwa na wananchi wameanza kurejea katika shughuli zao za kila siku kwa utulivu.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkerege, Joseph Mwita Ryoba, alisema kijiji hicho kilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na kilimo cha bangi, ambapo mwaka 2024 ekari zaidi ya 3,000 ziliteketezwa katika operesheni za serikali.
Alisema kwa sasa wananchi wengi wameachana na kilimo hicho na kuelekeza nguvu zao katika shughuli halali za uzalishaji, jambo linaloonesha kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment