NEWS

Friday 20 May 2022

Kampeni ya upandaji miti yapamba moto Musoma Vijijini, Mbunge Prof Muhongo agawa miche 10,000MBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo anashirikiana na VI Agroforestry Project ya AIC (African Inland Church) kupanda miche ya miti ikiwemo ya matunda katika vijiji, shule na madhehebu ya dini jimboni.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mbunge Muhongo inaeleza kuwa wakulima binafsi nao wanapewa miche ya miti kwa ajili ya kupanda.

Miche hiyo inatolewa bure na iwapo inapaswa kununuliwa (kama vile miche ya mivule), Mbunge huyo anainunua na kuigawa bure.Jumatano wiki hii, Mbunge Muhongo aliambatana na mtaalamu wa misitu, Jacob Malima wa VI Agroforestry Project kugawa miche 10,000 kwenye vijiji vilivyopo kando kando ya Ziwa Victoria (Kurwaki, Kiriba, Bwai Kumsoma) na Kisiwa cha Rukuba ambacho kilipata miche 4,500.

Mbunge Profesa Muhongo (kushoto) akigawa miche kwa baadhi ya wakazi wa Kisiwa cha Rukuba.

Aidha, mipango inawekwa na Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya upandaji mkubwa wa miche ya miti katika maeneo ya vijiji vyote 68 vinavyounda jimbo la Musoma Vijijini, ikiwemo milima ya Nyaberango na Mtiro ambayo kwa sasa ni ‘vipara vitupu’.

“Malengo yetu ni kupanda miche 100,000 wakati wa mvua za vuli za Oktoba 2022,” amesema Mbunge Profesa Muhongo katika taarifa hiyo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages