NEWS

Monday, 16 May 2022

Mgogoro wa viwanja Sirari watatuliwa Baraza la Madiwani Tarime Vijijini




HATIMAYE mgogoro wa kugombea viwanja namba 411, 412 na 413 vilivyopo kata ya Sirari, umepata ufumbuzi katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Viwanja hivyo vimekuwa vikigombewa na wafanyabiashara Peter Zakaria na Joseph Nyabaturi kwa ajili ya kujenga kituo cha mafuta ya magari.

Mkuu wa Idara ya Ardhi, Philip Marach, kwa idhini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati, alikieleza kikao hicho Ijumaa iliyopita, kwamba mmiliki halali wa viwanja hivyo ni Zakaria.

Marach alitangaza msimamo huo wa Halmashauri baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira, Godfrey Kegoye kukieleza kikao hicho kwamba walifanya ufuatiliaji ikabainika Nyabaturi ana nyaraka za kughushi kuhusu umiliki wa viwanja hivyo.

Aidha, alisema ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji imeshamwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi barua ya kutaka mtumishi aliyetengeneza nyaraka hizo za kughushi achukulie hatua za kinidhamu.



Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Samwel Kiles aliunga mkono hatua ya kutaka mtumishi huyo (hakutajwa jina) awajibishwe ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wanaochangia migogoro ya viwanja na ardhi katika jamii.

Ufumbuzi wa mgogoro huo ni matunda ya swali lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Sirari, Amos Sagara aliyetaka kujua mmiliki halali wa viwanja hivyo.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages