NEWS

Thursday 16 June 2022

IGP Sirro apangua vigogo wa Polisi mikoani, Tarime Rorya yaguswaMKUU wa Jeshi la Polisi (IGP) Tanzania, Simon Sirro (pichani), amefanya uhamisho wa baadhi ya maofisa ili kuboresha utekelezaji wa majukumu ya jeshi hilo.

Kulingana na taarifa ya kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Sirro amefanya uhamisho huo leo Juni 16, 2022.

Katika uhamisho huo, Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) William Mkonda amepelekwa kuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kuchukua nafasi ACP Abdi Isango anayekwenda kuwa Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mbeya.

Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mbeya, ACP Kennedy Mgani amepelekwa kuwa Mkuu wa Operesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kuchukua nafasi ya ACP Zuberi Mwombeji ambaye amehamishwa kwenda Makao Makuu ya Polisi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Uchumi.

Aidha, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Tarcis Idelfonce amehamishwa kwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dodoma, kuchukua nafasi ya ACP Pipi Kayumba ambaye amepelekwa kuwa Afisa Mnadhimu Namba Moja Mkoa wa Singida.

“IGP Sirro pia amemhamisha SSP Jumanne Juke aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita kwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, kuchukua nafasi ya ACP Ame Anoqie ambaye amehamishiwa Tarime Rorya kuwa Afisa Mnadhimu Namba Moja,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages