NEWS

Thursday 16 June 2022

Wadau wa maji Tarime wahimizwa kusimamia na kutekeleza miradi ya maji kwa welediVIONGOZI wa vyombo vya watumia maji, vijiji, kata na wataalamu wa maji katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, wamehimizwa kusimamia na kutekeleza miradi ya maji kwa weledi, ili iwe endelevu kwa manufaa ya wananchi.

Akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Maji Wilaya ya Tarime kwenye ukumbi wa TTC leo Juni 16, 2022, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Upendo Kasanga (pichani juu), amesema viongozi hao wana jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na Serikali kugharimia utekelezaji wa miradi ya maji.

Upendo amewakumbusha pia kusimamia usalama wa miradi ya maji, akionya kuwa Serikali haitamvumilia kiongozi mzembe na mtu yeyote atakayeharibu miundombinu ya miradi ya maji.

“Serikali inatumia fedha nyingi kugharimia miradi ya maji, hivyo haitafumbia macho vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za maji, uzembe wa viongozi kwenye suala la maji na uharibifu wa miundombinu miradi ya maji,” amesisitiza.

Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara, Marco Chogelo amewahamasisha ushirikiano na mawasiliano ya karibu baina ya vyombo vya watumia maji na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuepusha uharibifu wa miundombinu ya miradi ya maji wakati wa ujenzi wa barabara.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa RUWASA Mkoa wa Mara, Flora Meela amesisitiza kuwa wadau wa maji wanapaswa kushirikiana katika kulea vyombo vya watumia maji viweze kusimamia kwa ufanisi uendelevu wa miradi ya maji.

Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Raymond Mwema ameipongeza RUWASA kwa juhudi kubwa inazofanya kuwaboreshea wananchi huduma ya maji.

Mwema ambaye ni Diwani wa Kata ya Sabasaba ametumia nafasi hiyo pia kuwahimiza viongozi wa vijiji na kata kusimamia miradi ya maendeleo, ikiwemo ya maji kwa uwazi na weledi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Erasto Mbunga amewataka viongozi na wajumbe wa vyombo vya maji kuimarisha ukusanyaji wa mauzo ya maji ili yasaidie kuendeleza na kuboresha miradi ya maji kwenye maeneo yao.

“Bili za maji zilipwe kwa wakati… tunatakiwa kufikia lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo ya maji kichwani,” amesema Mbunga.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mohamed Mtopa, hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wilayani kwa sasa ni wastani wa asilimia 73.

“Kabla ya RUWASA kuanzishwa mwaka 2019, hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Tarime ilikuwa asilimia 47.5, ila baada ya miaka mitatu tumesogea hadi asilimia 73,” amesema.

Aidha, Mhandisi Mtopa amesema miradi ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni nne inaendelea kutekelezwa wilayani Tarime.

“Kwa sasa Tarime tunatekeleza miradi tisa na kwa bajeti inayokuja tutatekeleza miradi saba. Lengo kuu la Serikali kupitia Sera ya Maji ni kwamba kufikia mwaka 2025 wastani wa upatikanaji wa maji uwe asilimia 85 vijijini na 95 mijini,” Mhandisi Mtopa.

Ametoa rai kwa jamii kuendelea kutunza vyanzo vya maji, kuboresha miundoombinu yake na kuwapa wataalamu wa maji ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maji.

“Nitoe shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha na kutuamini watumishi wa Wizara ya Maji kuendelea kuchapa kazi. Vile vile nimpe kongole Mheshimiwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa jinsi anavyoongoza wizara na kutuamini sisi wataalamu katika utekelezaji wa miradi ya maji,” amesema Mhandisi Mtopa.

Mkutano huo umehitimishwa kwa mgeni rasmi kuwatunuku vyeti maalum viongozi wa vyombo vya maji vilivyofanya vizuri katika usimamizi wa miradi ya maji wilayani Tarime; ambavyo ni Nyamwaga, Sirari na Kewanja.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages