TAKRIBAN watoto 100 wenye ulemavu wamepewa mafunzo kuhusu haki zao na kujikinga na vitendo vya ukatlii wa kijinsia (GBV) katika halmashauri zote mbili za wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Mafunzo hayo yametolewa na Shirika la ATFGM Masanga leo Juni 15, 2022 kupitia mradi wake mpya unaolenga kusaidia watoto wenye ulemavu kupata haki zao, ikiwemo elimu, afya na ushirikishwaji, chini ya ufadhili wa Shirika la Terre des Homess la Uholanzi (The Netherlands).
Watoto walionufaika na mafunzo hayo ni kutoka halmashauri za wilaya ya Tarime (Vijiini) na Tarime Mji, huku wakisaidiwa kung’amua mafunzo hayo na mkalimani wa lugha za alama, Mwalimu Getrude Kilavo kutoka Shule ya Msingi Turwa iliyopo Tarime mji.
“Mbali na kujifunza kuhusu haki zao za msingi, wamepata mafunzo kuhusu mifumo ya kuwasaidia kutoa taarifa za ukatili,” amesema Afisa Ustawi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Ghati Okoth katika mazungumzo na Mara Online News, muda mfupi baada ya mafunzo hayo kuhitimishwa kwenye ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime, ambapo pia watoto hao wamepata fursa ya kuburudika na kupata chakula cha pamoja kabla ya kutawanyika.
Ghati amesema watoto hao wa kike na kiuume, wengine wapo shule na wengine wapo nje ya shule.
“Tunashukuru Shirika la ATFGM Masanga kwa mafunzo haya. Uelewa wa jamii kuwapa watoto wenye ulemavu haki zai ikiwemo elimu, afya na ushirikiswhaji ni jambo muhimu sana,” ameongeza Ghati.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Elimu Maalumu katika Halmashauri hiyo, Magreth Mwema amesema mafunzo husaidia kubadilisha maisha ya watoto wenye ulemavu.
“Uzoefu unaonesha kuna maendeleo ya watoto wenye ulemavu wanaopata elimu na mafunzo na ndio maana tunashukuru Shirika la ATFGM Masanga,” amesema Mwema na kuwataka wazazi/walezi wenye watoto wenye ulemavu kuhakikisha wanapata elimu.
Nao viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Wilaya ya Tarime wamesema mradi huo utakuwa na matokeo chanya kwa watoto wenye ulemavu.
“Tumepokea mradi na mafunzo haya kwa mikono miwili, utasaidia kutambua haki za watoto wenye ulemavu na kuzuia ukatili wa kijinsia kwa watu wenye ulemavu,” amesema Katibu wa SHIVYAWATA Halmashauri ya Tarime Mji, Mekaus Maingu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Watu Wenye Ulemavu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Riziki Focus utakuwa ni suluhisho la changamoto zinazowakbili watoto wenye ulemavu katika wilaya hiyo.
“Tumefurahi kuwa mradi huu sasa utasaidia kutambua idadi ya watoto wenye ulemavu walipo na kushawishi wazazi na walezi kuwapeleka kupata huduma kama vile elimu na afya badala ya kuwaficha,” amasema Riziki.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009, watoto wenye ulemavu wanastahili haki za kuishi kwa uhuru, kupewa jina, kucheza, kupata chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, kulindwa na kushirikishwa, miongoni mwa stahiki nyingine.
Shirika la ATFGM Masanga limesema mpango huo wa kutambua watoto wenye ulemavu pia utahushisha kuishawishi jamii kutunga sheria ndogo ndogo za kutetea na kulinda watoto haki zao.
Shirika hilo pia limejikita katika utoaji wa elimu ya madhara ya ukatili na unyanyasaji, ikiwemo ukeketaji, vipigo, mimba na ndoa za utotoni.
(Habari na picha: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment