Mwalimu wa Mazingira, Alexander Mhangate (katikati) akizungumzia upandaji miti katika Shule ya Sekondari ya Somoche wilayani Serengeti.
MAFANIKIO ya miradi ya uhifadhi vyanzo vya maji, misitu na mazingira, yameonekana katika vijiji mbalimbali mkoani Mara, vilivyopata misaada ikiwemo wa elimu husika kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF).
Watekelezaji wa miradi hii wanasema mafanikio hayo yamechochewa na Shirika la WWF, ambalo limekuwa mdau wao mkubwa katika uhifadhi huo.
Shule ya Sekondari ya Somoche iliyopo wilayani Serengeti, ni miongoni mwa wanufaika wa elimu ya utunzaji mazingira kwa njia ya upandaji miti na ufugaji nyuki, iliyotolewa na WWF.
Baadhi ya majengo ya Shule ya Sekondari ya Soomoche
“Wakati shule hii inaanzishwa mwaka 2019, eneo hili halikuwa na mti, lakini WWF kupitia Jumuiya ya Watumia Maji Somoche walituletea miche 500 ya miti tukapanda ikaota yote,” anasema Mwalimu wa Mazingira, Alexander Mhangate katika mazungumzo na Mara Online News shuleni hapo, wiki iliyopita.
Tangu wakati huo, walimu na wanafunzi wamehamasika na sasa suala la upandaji miti limekuwa endelevu katika shule hii.
“Hapa hata walimu; kila mmoja ana mti aliopanda, sasa hivi tuna miti takriban 2,000 ikiwemo ya matunda na kivuli, inapendezesha mazingira ya shule yetu,” anasema Mhangate.
Mwalimu Nicholaus Joshua akionesha mti alioupanda na kuendelea kuutunza shuleni hapo
Mkuu wa Shule hii, Mwalimu Nicholaus Joshua anasema ina wanafunzi zaidi ya 300 wa kidato cha kwanza hadi cha nne, na kila anayejiunga nayo lazima aripoti akiwa na miche mitano ya miti kwa ajili ya kuipanda na kuitunza.
Ufugaji nyuki
Kwa upande mwingine, Mhangate ambaye pia Mratibu wa mradi wa ufugaji nyuki shuleni hapo, anasema walianza na mizinga minane, lakini sasa wanayo 40, ikiwemo 32 ya kisasa na minane ya kienyeji.
“Hii mizinga 32 ya kisasa ni msaada tuliopata kutoka Mfuko wa Misitu Tanzania. Tumefikia hatua hii baada ya WWF kutupatia elimu ya ufugaji nyuki,” anasema.
Mwalimu Mhangate akionesha baadhi ya mizinga ya mradi wo wa ufugaji nyuki
Kupitia elimu na mradi huo, mwanafunzi wa kidato cha nne, Maseko Magita amehamasika kuanzisha ufugaji nyuki nyumbani kwao.
“Nimeamua kujishughulisha na ufugaji nyuki mpaka nyumbani kwa sababu unasaidia mimea kupata ushavushaji. Pia, ukifuga nyuki unakuwa unalinda mazingira, kwa sababu watu hawawezi kukata miti maeneo yaliyo na nyuki,” anasema Maseko.
Mwanafunzi huyo anasema alianza na mzinga mmoja, lakini kwa sasa anamiliki mizinga minane, ikiwemo saba ya kienyeji na mmoja wa kisasa, na kwamba amekuwa akirina asali kila baada ya miezi minne.
Maseko akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayupo pichani)
Hata hivyo, Maseko haridhishwi na soko la asali katika jamii inayomzunguka. “Watu wa huku hawapendi kununua asali, huwa nauza kidogo na nyingi huwa inatumika pale nyumbani,” anasema.
Matamanio yake ni kupata vitendea kazi, ikiwemo mizinga ya kisasa na vifaa vya kurinia asali, ili aweze kuwa mfugaji mkubwa wa nyuki Somoche baada ya kuhitimu masomo.
Wanufaika wengine wa elimu ya ufugaji nyuki na uhifadhi mazingira wilayani Serengeti iliyotolewa na WWF, ni Kikundi cha Kegonga.
Mwenyekiti wa Kikundi hiki, Daniel Mawe anasema wanamiliki mizinga 10 ya nyuki, chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Watumia Maji Kegonga.
Daniel Mawe akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayupo pichani)
“Mradi huu umesaidia kurejesha hifadhi ya msitu iliokuwa hatarini kutoweka, tunaishukuru WWF kwa kutuwezesha kufikia hatua hii,” anasema mwanachama wa kikundi hicho, Sarah Mbota.
Upimaji mito
WWF pia imeipatia Shule ya Sekondari ya Somoche elimu ya awali na vitendea kazi vya kupima afya ya mito kupitia wadudu wanaoishi majini.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hii wanaounda kikundi cha upimaji afya ya maji, Hamis Marwa anasema wanafanya shughuli hizo kipindi cha kiangazi na masika na kwamba matokeo ya upimaji wanayapeleka ofisi za Bonde la Mto Mara na Ziwa Victoria kwa hatua za kitaalamu zaidi.
Wanafunzi shule hiyo wakipima afya ya mto
Shule hii imenufaika pia na msaada wa tenki la lita 5,000 kutoka WWF, kwa ajili ya kuvunia maji ya mvua.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu, Veronica Nyamhanga anasema tenki hilo linawasaidia wanafunzi na walimu kuvuna na kuhifadhi maji ya matumizi mbalimbali, ikiwemo kunywa na kumwagilia miti inayooteshwa shuleni hapo.
“Tunaishukuru WWF kutuletea tenki, sasa tunavuna maji, japo hayakidhi mahitaji ya shule, tunaomba ikiwezekana watuongeze matenki manne maana wanafunzi wanaongezeka kila mwaka,” anasema Veronica.
Veronica Nyamhanga
Mwenyekiti wa Jumuia ya Watumia Maji Somoche, Matinde Ibrahim anasema juhudi zaidi zinahitajika kuelimisha wakazi wa eneo hilo kuhusu umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji, misitu na mazingira kwa ujumla.
Uoteshaji miche
Juhudi za WWF pia zimeonekana wilaya ya Butiama, ambapo imewezesha Jumuiya ya Watumia Maji Mara Kusini kuanzisha mradi wa uoteshaji miche ya miti kwa ajili ya kujipatia kipato na kuhifadhi mazingira.
Mwenyekiti wa Jumuiya hii, Mahiri Magabe anasema wanatumia Kamati ya Maji kusimamia kikundi kinachoendesha mradi huu kijijini Kwisaro.
“WWF wamekuwa wadau wetu wakubwa kuanzia kwenye elimu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira hadi vitendea kazi, ikiwemo msaada wa tenki la lita 5,000 la maji ya kumwagilia vitalu vya miche na kulijengea uzio wa nyaya,” anasema Magabe.
Hapa shughuli za kikundi hicho zikiendelea
Magabe anaongeza “Kwa sasa tuna mipango ya kuotesha miche 40,000 na baadaye ufugaji nyuki kwa ajili ya kuuzia taasisi mbalimbali zikiwemo shule na kutunza mazingira. Lengo letu ni kuondoa jamii kwenye uharibifu wa mazingira.”
Mwanachama wa kikundi hiki, Mwanne Wilson anasema uhamasishaji wao umesaidia kubadilisha mazingira kwa ongezeko la misitu katika vijiji vinane vilivyo ndani ya jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maji katika eneo hili, Tatu Steven anasema “Fedha tunazopata kwa kuuza miche ya miti zinatusaidia hata sisi akina mama kununua mbuzi wa kufuga na mahitaji mengine, kama vile magodoro ya kulalia.”
Mahiri Magabe (kulia) akizungumza na ofisa wa WWF, Matilda Sefukwe kijijini Kwisaro
Usomaji maji
Wilayani Tarime, WWF imewezesha uanzishaji kituo cha kusoma wingi wa maji ndani ya Jumuiya ya Watumia Maji Tigithe Juu.
Kiongozi wa kituo hiki, Juma Kiboye anasema wanasoma wingi wa maji ya mto Tigithe mida ya asubuhi na jioni kila siku, mwisho wa mwezi hupeleka taarifa ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria na Dakio Dogo la Mto Mara.
“Lakini pia WWF ilitupatia elimu ya kupima afya ya mto wakati wa kiangazi na masika. Kuna wadudu ambao tukikutana nao tunajua huu mto si salama,” anasema Kiboye.
Kiboye kazini
Kiboye anaongeza kuwa WWF pia imeanzisha klabu za wanafunzi wa shule mbalimbali, ikiwemo sekondari ya Bwirege, shule za msingi Keisangora na Kangariani kujihusisha na utunzaji mazingira shuleni na vyanzo vya maji.
“WWF pia wametuwezesha kupanda miti iliyo rafiki kwenye maeneo ya vyanzo vya maji vikiwemo visima vya Bilili na Nyitembe, na kuweka vigingi kwa umbali wa mita 60 kutoka vyanzo vya maji kuzuia shughuli za kibinadamu,” anasema Kiboye.
Ufugaji samaki
Matunda ya elimu inayotolewa na WWF yameonekana pia katika kijiji cha Nyakunguru wilayani Tarime, hususan kwenye Kikundi cha Ufugaji Samaki cha Mtalimbo.
Kikundi hiki kinaendeshwa chini ya Mwenyekiti, Zuhura Masanga na Wakurugenzi, Bigambo Maximilian na Joseph Moya. Wanasema walianza kufuga samaki aina ya kambale, lakini kwa sasa wamejikita kwenye aina ya sato kwenye mabwawa.
“Sasa hivi tumeanza kuzalisha wenyewe vifaranga vya samaki aina ya sato ili tuwe na uvunaji endelevu wa samaki hawa,” anasema Bigambo.
Mkurugenzi Bigambo (katikati) akiwaeleza maofisa wa WWF maendeleo ya Kikundi cha Ufugaji Samaki Mtalimbo
Meneja Mradi wa Kikundi hiki, Laylat Maximilian anasema hadi sasa wanafuga maelfu ya samaki hao kwenye mabwawa manne.
Laylat anasema mbali na kuwa chanzo chao cha mapato, kuchangia uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira, mradi huu unatoa ajira zikiwemo ndogo ndogo kwa vijana kijijini hapo.
Laylat akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayupo pichani)
Mkazi wa kijiji cha Nyakunguru, Vincent Moya anasema yeye na vijana wenzake wamekuwa wakipata ajira ya muda, ikiwemo kuchimba mabwawa ya samaki.
Ndoto za Kikundi cha Mtalimbo ni kuwa mfugaji mkubwa wa samaki ili pia kiweze kukidhi mahitaji ya soko linalopatikana Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
“WWF wametubeba sana katika mradi huu, walipeleka mwanakikundi mwenzetu [Joseph Moya] kupata mafunzo ya ufugaji nyuki nchini Uganda. Matokeo ya jitihada za shirika hili yamekuwa mazuri kwetu,” anasema Mkurugenzi Bigambo.
Joseph Moya akionesha kifaa cha kupima upepo kwenye mojawapo ya mabwawa yao ya kufugia samaki
WWF wanena
Afisa Mradi wa WWF Mara, Kanuni Kanuni anasema jukumu lao kubwa ni kuwapa wananchi elimu ya uhifadhi na utunzaji vyanzo vya maji na mazingira hai katika dakio dogo la Mto Mara.
“Tumejikita kwenye uhifadhi wa mto Mara, tunafanya kazi kwa ukaribu na jumuiya za watumia maji na kamati za maji, hususan katika uhifadhi, ulinzi wa mazingira na vyanzo vya maji, ikiwemo mito Tigithe na Somoche,” anasema Kanuni.
Kanuni akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayupo pichani)
Wiki iliyopita, maofisa kutoka WWF Makao Mkuu Dar es Salaam, Matilda Sefukwe (Kingo cha Tathmini na Ufuatiliaji) na Joan Itanisa (Mawasiliano), walitembelea na kuridhishwa na maendeleo ya miradi ya utunzaji mazingira katika vijiji vilivyonufaika na elimu iliyotolewa na shirika hilo.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment