NEWS

Saturday 18 June 2022

Viongozi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti wammwagia sifa Rais Samia kuwapatia gari jipya la TASAF



MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma (pichani kulia), amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia halmashauri hiyo gari jipya kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini.

Gari hilo ni miongoni mwa 241 yaliyotolewa na Rais Samia kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo nchini.

“Ninamshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutupatia gari jipya kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa vizuri katika halmashauri yetu,” amesema Makuruma wakati wa mapokezi ya gari hilo katika halmashauri hiyo jana.

Amesema gari hilo litaongeza ufanisi katika utekelezaji wa mpango huo kwenye vijiji 74 na vitongoji 17 vinavyolengwa katika halmashauri hiyo.

Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe kwa tiketi ya chama tawala - CCM, amelezea kufurahishwa na namna ambavyo Rais Samia ameendelea kuwajali watu wa Serengeti katika suala zima la maendeleo.

“Mtakumbuka kwamba ni hivi karibuni kupitia ule mpango wa COVID-19 tulipata madarasa 119 katika halmashauri yetu, lakini vile vile iko miradi mingine mikubwa ambayo imeendelea kutekelezwa hapa, ambayo nikichukua yote ni zaidi ya shilingi bilioni 7.7 ambazo zimekwisha kuingia katika halmashauri yetu.

“Kwa hivyo unaweza kuona ni namna gani Rais wetu Samia anavyoendelea kutusaidia, kushirikiana nasi na anavyoendelea kuwapenda watu wa Serengeti.

“Ninamshukuru sana Rais Samia kwa kuendelea kusikiliza kilio chetu na kuendelea kutusaidia, ukiangalia tumekuwa miongoni mwa halmashauri za mwanzo kabisa kupata gari hili.

“Kwa niamba ya halmashauri yetu niseme kwamba tunamwombea kila la heri Rais wetu aendelee kuliongoza taifa letu kwa amani na ustawi mkubwa.

“Tunamshukuru sana kwa jambo hili, nikimwombea kwa Mungu aendelee kumsaidia ili aendelee kutukumbuka zaidi na zidi, kwa sababu changamoto bado tunazo nyingi, lakini kwa namna hii maana yake ni kwamba kadiri kunavyokucha tumeendelea kuona chini ya uongozi wake, changamoto hizi zikipungua moja baada ya nyingine.

“Ninaamini sasa walengwa watafikiwa vizuri, kwa ukamilifu zaidi na wataendelea kutengeneza maisha yao kupitia mpango huu wa TASAF,” amesema Makuruma.

Naye Mratibu wa TASAF Wilaya ya Serengeti, Ntusa William (pichani juu katikati), amemshukuru Rais Samia akisema gari hilo litawarahisishia shughuli za kuwafikia na kuwahudumia walengwa kwa wakati vijijini.

“Halmashauri yetu kwa muda mrefu imekuwa na changamoto ya usafiri, hasa katika kuwafikia walengwa wa mpango huu,” Ntusa amesema na kuahidi kuwa watalitumia gari hilo kwa kuzingatia taratibu na maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali.

Kwa mujibu wa Ntusa, Halmashauri ya Wilaya ya ina walengwa 4,017 wa TASAF katika vijiji na vitongoji 91.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages