NEWS

Saturday 18 June 2022

Siku ya Mtoto wa Afrika: Right to Play, AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe waadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuandaa tamasha la michezo kwa wanafunzi, wahamsisha fursa sawa ya elimu kwa watotoSHIRIKA la Right to Play limeshirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, kwa kuandaa tamasha maalum la michezo mbalimbali kwa wanafunzi katika Shule ya Msingi Gwitare wilayani Tarime.

Washindi wa michezo hiyo, ikiwemo mpira wa miguu na kuvuta kamba kwa wasichana na wavulana, walipewa zawadi za vikombe na madaftari.

Akizungumza katika tamasha hilo, Afisa Mrdi kutoka Knisa hilo AICT, Rebeca Bugota amesema wanashirikiana na Right to Play kuhamasisha masuala ya kielimu kwa watoto walio shuleni kijijini Gwitare.

Rebeca (kulia) na viongozi wengine wakibidhi zawadi ya kombe kwa wanafunzi walioibuka washindi katika mashindano hayo.

“Shirika la Right to Play linafanya jitihada nyingi kuhakikisha mtoto anaongeza uwezo wake wa kusoma, na linawapa watoto wote; wa kike, wa kiume na wenye ulemavu fursa sawa ya kupata elimu.

“Hapa Gwitare tunasaidia masuala ya kielimu ili kuona mwamko wa elimu mahali hapa unakuwa mzuri na watoto wanatimiziwa mahitaji yao yote,” amesema Rebeca.

Ameongeza kuwa mashirika hayo pia yanawasaidia watoto kuwa na stadi za maisha kupitia kituo cha usomaji kilichopo Gwitare siku za Jumatano na Ijumaa.

“Kwa hiyo wazazi mliopo hapa wapeni watoto nafasi ya kusoma kwa sababu elimu ndiyo inaweza kuwasaidia watakapokuwa wakubwa wasiwe tegemezi, walifae taifa letu kwa maendeleo,” amesema.

Naye Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Gwitare, Godfrey Denis amesema Shirika la Right to Play limewasaidia mambo mengi, hasa kuelimisha jamii kuepuka ukatili kwa watoto na namna bora ya kuwasaidia katika masomo.


“Tunashukuru tumekuwa nao katika tamasha hili, tumeweza kuelimisha jamii juu ya namna ya kumlinda mtoto na kuangalia haki za mtoto, tunaomba waendelee kuwepo kwa ajili ya kusaidia jamii,” amesema Mwalimu Denis.

Ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa jamii kuwapa watoto wa kike elimu na kuacha kuwakeketa.

Right to Play ni shirika la kimataifa lililopo Canada, linalosaidia watoto na vijana kujikomboa kutoka kwenye matatizo mbalimbali, na linafanya kazi katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.

Kwa Tarime, linawasaidia watoto, hususan wanaosoma shule za msingi, ili waweze kukuza uwezo wao wa kusoma.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages