NEWS

Monday 11 July 2022

Mbunge Waitara aipongeza JK Nyerere kwa kung’ara matokeo kidato cha sita Tarime Vijijini, aiahidi msaada wa TV na king’amuzi



MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, ameipongeza Shule ya Sekondari JK Nyerere kwa kufanya vizuri kwenye matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Kidato cha Sita mwaka huu (2022) na kushika nafasi ya kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Akizungumza katika hafla fupi shuleni hapo leo Julai 11, 2022, Mbunge Waitara amesema wanafunzi, walimu, wazazi na walezi husika wanastahili pongezi kubwa kutokana na ushindi huo.

Mbunge Waitara akizungumza katika hafla hiyo

Mbunge huyo ametaka ushindi huo uwe chachu kwa wanafunzi waliobaki na walimu wa shule hiyo kuongeza bidii ya kufanya vizuri zaidi kitaaluma.

Katika kuonesha kufurahishwa na ushindi huo, Mbunge Waitara amewapatia wanafunzi wa kidato cha tano hadi cha sita na walimu wao, shilingi 340,000 ikiwemo 100,000 aliyoungwa na Diwani wa Nyamwaga, Mwita Magige, kwa ajili ya kununua mchele, nyama na soda.

Aidha, Mbunge huyo ameahidi kuipatia shule hiyo msaada wa TV na kingamuzi kwa ajili ya kutazama taarifa za habari, zikiwemo za michezo, vipindi vya Bunge na matukio mengine.

Katika hatua nyingine, amesema Halmashauri inasubiri Mkuu wa Mkoa wa Mara aruhusu fedha za CSR iweze kumega shilingi milioni 60, kwa ajili ya kugharimia ukamilishaji wa bweni la pili shuleni hapo, ili kuwaondolea wanafunzi wa kidato cha tano na sita (ambao wote ni wasichana) msongamano wa kulala wawili wawili kwenye kitanda.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari JK Nyerere, Mwalimu Melesian Gerald, amemwambia Mbunge Waitara kuwa shule hiyo imekuwa ya kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) na ya pili kiwilaya, ikitanguliwa na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tarime.

Mwalimu Melesian akizungumza katika hafla hiyo

Mwalimu Melesian amesema JK Nyerere imefuatiwa na shule za sekondari Ingwe, Magoto, Manga na Borega katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Kidato cha Sita mwaka huu.

(Habari na Picha: Sauti ya Mara Digital)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages