NEWS

Thursday 7 July 2022

Mfanyabiashara Nyabaturi akabidhi msaada wa darasa la kisasa Shule ya Getagasembe wilayani Tarime



MFANYABIASHARA Joseph Nyabaturi, amekabidhi msaada wa chumba cha darasa la kisasa alichojenga kwa gharama ya shilingi milioni 20 (pichani juu) na ofisi ya Mwalimu Mkuu aliyokarabati kwa shilingi milioni 1.5 katika Shule ya Msingi Getagasembe iliyopo kata ya Gwitiryo wilayani Tarime, Mara.

Nyabaturi ambaye ni Mkurugenzi wa miradi ya kiuchumi ya Serengeti Tower na Sirari Food katika mji wa Sirari mpakani na nchi ya Kenya, amekabidhi msaada huo kwa viongozi wa shule hiyo, kijiji cha Getagasembe na kata ya Gwitiryo, jana Julai 6, 2022.

“Nimetoa msaada huu ili kuunga mkono juhudi za Serikali na kuwapunguzia wazazi mzigo wa kutoa michango ya maendeleo ya shule hii, lakini pia nimeweka kumbukumbu kwenye shule niliyosoma.

“Ningesema ninunue gari ningetembelea mimi na familia yangu, lakini sasa nimesaidia wanakijiji wenzangu na jamii yangu, hapa watapita watu wengi, vizazi vingi vitapita kupata elimu,” amesema Nyabaturi.

Kuhusu ukarabati wa ofisi ya Mwalimu Mkuu, Nyabaturi amesema “Baada ya kujengea wanafunzi darasa, nikaona ofisi ya mwalimu haina kigae wakati darasa la mwanafunzi lina kigae, nikaona nitakuwa nimefanya ubaguzi, hivyo nikaona na mwalimu naye nimrekebishie ofisini kwake pakae vizuri.”

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo amesema binafsi anaona msaada huo ni wa kawaida na kwamba anaweza kusaidia mahitaji mengine ya shule hiyo kadiri atakavyoweza.

“Sio kwamba nimefnya kitu kikubwa sana, bado likihitajika jambo jingine nililo na uwezo nalo nitakuja kufanya kama mwanakijiji,” amesema Nyabaturi.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wakazi wa kijiji cha Getagasembe na kata ya Gwitiryo kuwa tayari kujitolea kuchangia maendeleo ya shule hiyo kwa chochote wanachoweza.

“Unaweza ukaja hata na miti ukapanda kwenye eneo la shule ili kulinda mazingira. Usisubiri upate hela nyingi ndio uje kujenga darasa, mchango ni sawa na sadaka, sadaka haiangalii nimetoa laki moja wewe umetoa elfu moja, inawezekana utakuwa umetoa zaidi yangu,” amesisitiza.



Wakizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Getagasembe, Hamis Mwita, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Sylvester Itembe, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Costantine Marwa, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Gwitiryo, Hidaya Peter na Diwani wa Kata hiyo, Mchuma Nashon wamemshukuru Nyabaturi kutokana na msaada huo.

“Tunamshukuru sana ndugu Joseph Nyabaturi, tunaomba wadau wengine waige mfano wake, wajitokeze kuchangia maendeleo ya shule hii kwani bado ina mahitaji mengi, bado tuna ufungufu wa vyumba vya madarasa, madawati na nyumba za walimu,” amesema Diwani Mchuma.


Diwani Mchuma (aliyesimama) akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo. Wa pili kushoto waliokaa ni mfanyabiashara Joseph Nyabaturi.

(Habari na picha: Sauti ya Mara Digital)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages