NEWS

Sunday, 4 January 2026

Maendeleo: Mwenyekiti mpya Halmashauri ya Bunda Mji ataja vipaumbele vyake



Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Masalo Minza Shani.

Na Mwandishi Wetu
---------------------------

Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, Masalo Minza Shani, ameweka wazi dira na vipaumbele vya maendeleo atakavyovisimamia ili kuimarisha huduma za kijamii na ustawi wa wananchi wa halmashauri hiyo.

Amesema uongozi wake utakuwa wa mipango yenye tija inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku akisisitiza uwajibikaji, ushirikishaji wananchi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Kipaumbele cha kwanza kitakuwa ni kuboresha huduma za jamii, hususan sekta ya afya kwa kuimarisha vituo vya afya na zahanati, kuhakikisha upatikanaji wa dawa na kuongeza idadi ya watumishi wa afya.

Katika sekta ya elimu, ataelekeza nguvu kwenye ujenzi na ukarabati wa shule, nyumba za walimu na kuongeza vifaa vya kujifunzia ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

“Upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa Bunda utaendelea kuwa ajenda ya msingi ili kuboresha afya na ustawi wa wananchi,” alisema Masalo katika mahojiano maalum na Mara Online News hivi karibuni.

Kwa upande mwingine, alisema barabara za mjini na mitaani, mifereji ya maji ya mvua pamoja na taa za barabarani zitaboreshwa ili kuendana na ukuaji wa mji.

Pia, atasimamia kwa karibu mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kudhibiti ujenzi holela na kuboresha mandhari ya mji, sambamba na kuimarisha miundombinu ya masoko, stendi na maeneo ya biashara.

Akizungumzia uchumi wa wananchi, Mwenyekiti huyo alisisitiza uwezeshaji wa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Hatua hiyo, alisema itaambatana na kukuza biashara ndogo na za kati, sekta isiyo rasmi na kushirikiana na sekta binafsi kuvutia uwekezaji katika biashara, utalii na viwanda vidogo.

Vilevile, alisema atahakikisha halmashauri inaendelea kuwasaidia wakulima kwa pembejeo, elimu ya kilimo bora na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

“Katika ufugaji, mkazo utawekwa kwenye ufugaji wa kisasa na kudhibiti magonjwa ya mifugo, huku sekta ya uvuvi ikipewa msukumo kupitia uvuvi endelevu na uhifadhi wa rasilimali za Ziwa Victoria,” alisema Masalo.

Kwa upande wa utawala bora, Masalo aliahidi kuimarisha uwazi na uwajibikaji, kupambana na rushwa na kusimamia matumizi sahihi ya mapato ya ndani na ruzuku za serikali.

Alisisitiza kuwa wananchi watashirikishwa kikamilifu kupitia mikutano ya hadhara na kamati za mitaa ili maamuzi ya maendeleo yawe shirikishi.

Aidha, alisema ajira kwa vijana zitakuzwa kupitia miradi ya maendeleo na uwekezaji, pamoja na kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya ufundi na ujasiriamali.

“Sekta ya michezo, sanaa na utamaduni pia itazingatiwa kama chanzo cha ajira,” aliongeza Masalo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mcharo.

Kuhusu mazingira, alisema halmashauri itasimamia usafi wa mazingira, ukusanyaji wa taka, uhifadhi wa vyanzo vya maji, upandaji miti na kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko.

Masalo alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani na usalama kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na jamii, kupambana na dawa za kulevya, vitendo vya ukatili na uhalifu, sambamba na kuhamasisha maadili, mshikamano na uzalendo.

“Maendeleo ya Halmashauri ya Mji wa Bunda yatawezekana endapo tutafanya kazi kwa pamoja, kwa uwazi na kwa kujali maslahi ya wananchi,” alisisitiza Masalo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages