NEWS

Tuesday 26 July 2022

Mgodi wa Barrick North Mara waiomba Serikali kuusaidia kutatua changamoto zinazoukabili



Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
----------------------------------------

KAMPUNI ya Barrick imewasilisha serikalini changamoto kubwa zinazoikabili katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

Meneja Mkuu (GM) wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko amewasilisha changamoto hizo kwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi alipofanya ziara ya kikazi mgodini hapo, Jumatano iliyopita.

GM Lyambiko ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ucheleweshaji kibali cha kuongeza eneo la bwawa la maji taka.

“Tulitakiwa kupata kibali Mei mwaka huu lakini hadi sasa hatujafanikiwa,” Lyambiko amemweleza RC Hapi, ingawa alisema majadiliano ya kukipata kutoka Wizara ya Madini yanaendelea.


GM Lyambiko akitambulisha wafanyakazi wa mgodi wa North Mara kwa RC Hapi (hayupo pichani)

Meneja huyo amesema ucheleweshaji huo ukiendelea unaweza kusimamisha uzalishaji wa dhahabu katika mgodi huo ifikapo mwakani.

Mmoja wa maofisa wa Serikali waliofuatana na RC Hapi katika ziara hiyo amesema kuna vitu ambavyo wanataka kujiridhisha navyo kabla ya kutoa kibali hicho.

“Kuna vitu ambavyo tunataka kujiridisha navyo na masharti ni kwamba wajenge TSF nyingine,” amesema ofisa huyo.

Akijibu hoja hiyo, GM Lyambiko amesema Barrick ina dhamira ya kujenga TSF mpya lakini suala la kupata kibali kwa sasa ni muhimu wakati maandalizi yanaendelea. “Tumedhamiria kujenga TSF mpya na tumetoa ratiba ya kufanya hivyo,” amesema.

Changomoto ya pili inayokabili mgodi huo kwa sasa amesema ni baadhi ya watu kugoma kuchukua hundi za malipo ya fidia za mali zao waweze kuondoka jirani na mgodi.


GM Lyambiko (kushoto) akimuonesha RC Hapi (katikati) mojawapo ya changamoto zinazoukabili mgodi wa North Mara

“Udhamini umefanyika lakini baadhi ya watu wamegoma kuchukua hundi zao. Tusaidie wachukue hundi zao ili waondoke kwenye maeneo ya mgodi,” GM Lyambiko amemuomba Mkuu wa Mkoa.

Ametaja changamoto ya tatu kuwa ni watu wanaovamia mgodi kwa ajili ya kupora mawe ya dhahabu huku wakiwa wamejihami kwa silaha za jadi, zikiwemo mapanga, mawe na mikuki.

“Tumefanya kamapeni ya kuwaomba wananchi waache kuvamia mgodi na imesaidia kupunguza uvamizi, lakini bado ni changamoto,” amesema Lyambiko.

Pia amesema kuna changomoto ya kutegesha ya miti, mazao na nyumba katika maeneo yanayohitajika kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za mgodi.

RC Hapi ameeleza kusikitishwa na vitendo vya tegesha na uvamizi unaofanywa na baadhi ya watu katika mgodi huo na kuahidi kutafuta suluhisho.


RC Hapi akisisitiza jambo kwa GM Lyambiko

Aidha, kiongozi huyo wa mkoa ameahidi kwamba Serikali itaendelea kutoa ulinzi mkali katika mgodi huo.

“Nataka niwahakikishie kuwa usalama wa mgodi huu utakuwa wa kiwango cha juu, na hayo ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais,” amesisitiza RC Hapi ambaye ziara yake katika mgodi huo ilichukua saa zaidi ya nne.

Amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushughulikia watu aliowaita wezi mapapa wa mawe ya dhahabu katika mgodi huo, badala ya kujikita kwa dagaa (wezi wadogo) pekee.

RC Hapi ametumia nafasi hiyo pia kuupongeza mgodi wa North Mara kwa shughuli kubwa za uchimbaji wa madini ya dhababu zinazotoa ajira kwa Watanzania.

Katika ziara hiyo, RC Hapi amefuatana na kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya mkoa, wilaya na maofisa wengine wa Serikali wakiwemo kutoka idara za ardhi, maji na madini.


Sehemu ya mgodi wa North Mara

North Mara ni mmoja ya migodi mikubwa nchini Tanzania - unaotengeneza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa maelefu ya Watanzania, sambamba na kuchangia mapato ya Serikali na maendeleo ya jamii inayouzunguka kupitia Mpango wa Uwajibikaji kwaa Jamii (CSR).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages