NEWS

Tuesday 26 July 2022

Wanakijiji Nyakunguru walalamikia uhamishaji wa mamilioni ya fedha zao kinyemela



Na Mwandishi Wetu, Tarime
-----------------------------------

WAKAZI wa kijiji cha Nyakunguru wamelalamikia kitendo cha kuhamisha shilingi milioni 75 za kijiji hicho kinyemela kwenda kijiji jirani cha Nyarwana.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapo Alhamisi iliyopita, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Chacha Makuri amesema fedha hizo ni ambazo zilitolewa na Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, chini ya Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).



Makuri amesema fedha hizo zilizokuwa zimeelekezwa kwenye mradi wa shule ya msingi tarajiwa ya Nyankorambe, zimehamishwa kwenda Shule ya Msingi Monanka iliyopo kijijini Nyarwana bila wakazi wa kijiji cha Nyakunguru kushirikishwa.

Hata hivyo, wana-Nyakunguru wanamtuhumu Diwani wao wa Kata ya Kibasuka, Thomas Nyagoryo kuwa ndiye aliyehusika kuwafanyia hujuma hiyo ya maendeleo ya kijiji chao.



Aidha, wameiomba ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Wizara yenye dhamana ya Serikali za Mitaa - TAMISEMI kuingilia kati ili fedha hizo zirejeshwe kijijini Nyakunguru kwa ajili ya kugharimia miradi iliyolengwa.

Tayari Mwenyekiti Makuri amemwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo barua ya malalamiko na kumuomba awasaidie ili fedha hizo zirejeshwe kijijini kwao.

Sauti ya Mara Digital inaendelea na juhudi za kuwapata Diwani wa Kibasuka na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa ajili ya ufafanuzi wa suala hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages