NEWS

Saturday 2 July 2022

TAKUKURU yawafikisha mahakamani Mtendaji wa Kijiji, Afisa Maendeleo na mfanyabiashara kutokaTarime na Rorya kwa uhujumu uchumiTAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKU) Wilaya ya Tarime, imewafikisha mahakamani watumishi wawili na mfanyabiashara kwa makosa ya udanganyifu, kugushi, ufujaji na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za Serikali.

Washtakiwa hao ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Genkuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Gichogo Chacha Nyankena anayekabiliwa na mashtaka matatu; ambayo ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, ufujaji na ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara.

Akisoma Shauri la Uhujumu Uchumi Namba 22/2022 la mashtaka hayo Julai 1, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Vicencia Balyaruha, Mwenyesha Mashtaka wa TAKUKURU na Wakili wa Serikali, Mwinyi Yahaya amedai Afisa Mtendaji huyo alitenda makosa hayo Agosti 16, 22 na 23, 2019 yaliyohusisha shilingi milioni 7.1 za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Wakili Yahaya amesema makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [Sura ya 329 mapitio ya 2019], vikisomwa pamoja na aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza pamoja na kifungu cha 57(I) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi [Sura ya 200 mapitio ya 2019].

Hata hivyo, Afisa Mtendaji huyo amekana mashtaka yote na amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili watumishi wa umma wanaoaminika wa kusaini bondi ya shilingi milioni 10 kila mmoja. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 14, 2022 kwa ajili ya kusikilizwa mahakamani hapo.

Wengine ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Felician Msira Meena na mfanyabiashara wa wilayani hapo, Amani Idi Ngajeni, wanaoshtakiwa kwa makosa matano, ambapo shtaka la pili linawahusu wote wawili na manne yanamhusu Afisa Maendeleo huyo.

Mashtaka hayo matano yametajwa kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kula njama za kutenda kosa, kughushi, ufujaji na ubadhirifu.

Kosa la kughushi ni kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu [Sura ya 16 mapitio ya 2019].

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU na Wakili wa Serikali, Mwinyi Yahaya akisoma Shauri la Uhujumu Uchumi Namba 23/2022 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Yohana Charles Myombo, Julai 1, 2022 amedai washtakiwa hao walitenda makosa hayo Machi 8 na 29, 2018 yanayohusisha shilingi 9,014,250 za Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.

Washtakiwa wote wamekana kutenda makosa hayo na wameachiwa kwa dhamana hadi Agosti 1, 2022 kwa ajili ya usikilizaji wa kesi hiyo mahakamani hapo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages