NEWS

Wednesday 20 July 2022

RC Hapi afanya ziara Barrick North Mara, aahidi ulinzi mkali mgodini
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
----------------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi (pichani juu katikati) leo Julai 20, 2022 amefanya ziara kwenye Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na kuahidi usalama wa hali ya juu katika mgodi huo wa Kampuni ya Barrick uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

“Nataka niwahakikishie kuwa usalama wa mgodi huu utakuwa wa kiwango cha juu, na hayo ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais,” amesisitiza RC Hapi baada ya kutembelea maeneo mbalimbali mgodini hapo.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amekemea vitendo vya uvamizi na wizi wa mawe yenye dhahabu mgodini hapo, akisema Serikali itashirikiana na mgodi kuvikomesha.

Ametaka vyombo vya ulinzi na usalama kushughulikia watu aliowaita wezi mapapa wa mawe ya dhahabu mgodini hapo, badala ya kujikita kwa dagaa (wezi wadogo) pekee.

RC Hapi ametumia nafasi hiyo pia kuupongeza mgodi wa North Mara kwa shughuli kubwa za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinazotoa ajira kwa Watanzania.

Awali, kiongozi huyo wa mkoa amepokewa na Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko ambaye ametoa taarifa za uendeshaji wa shughuli za mgodi huo.

Meneja Mkuu, Apolinary Lyambiko (kulia) akitambulisha wafanyakazi wa mgodi huo

Mbali na kutembelea eneo la bwawa la kuhifadhi maji taka (TSF), RC Hapi pia amepata fursa ya kujionea shughuli za uchimbaji wa mawe ya dhabau kwenye mashimo ya wazi na chini ya ardhi mgodini hapo.


Pamoja na mambo mengine, Meneja Mkuu, Lyambiko, ameiomba Serikali kupitia kwa Mkuu huyo wa mkoa kuusaidia mgodi huo kudhibiti uvamizi na wizi wa mawe ya dhahabu mgodini.

Kuhusu watu wliogoma kuhama ili kupisha shughuli za mgodi baada ya kufanyiwa tathmini, Lyambiko ameiomba Serikali kusaidia kuwashawishi wakubali kupokea hundi za malipo ya fidia za mali zao na kuondoka jirani na mgodi.

Pia ameomba Serikali kuuwahishia mgodi huo kibali cha kuongeza eneo la kumwaga maji taka.


Kuhusu vitendo vya kutegesha miti, mazao na nyumba katika maeneo yanahitajika kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za mgodi huo, RC Hapi amesema Serikali italifanyia kazi ili kuhakikisha mambo yanakaa vizuri.

Katika ziara hiyo, RC Hapi amefuatana na kamati za ulinzi na usalma ngazi ya mkoa, wilaya na maofisa wengine wa Serikali, wakiwemo wa ardhi, maji na madini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages