NEWS

Saturday 16 July 2022

RC Mara aipa kongole Halmashauri ya Tarime Mji



MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Salum Hapi (pichani juu), ameitaja Halmashauri ya Mji wa Tarime kama moja ya halmashauri za mfano kwa utulivu na uchapa kazi katika mkoa huo uliopo Kanda ya Ziwa.

“Kwa kweli katika halmashauri ambazo zimetulia ni pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tarime,” RC Hapi amesema katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo mjini hapa, Jumatano iliyopita.
RC Hapi amesema halmashauri hiyo imeweza kukusanya mapato kwa asilimia 97 kwa mwaka wa fedha uliopita.

“Pokeeni pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” Hapi amewambia madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo.

Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa sasa ipo chini ya uongozi wa Mwenyekiti Daniel Komote na Mkurugenzi, Gimbana Ntavyo.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo kikamilifu ili kutekelesza ilani ya chama tawala - CCM kwa ufanisi katika ngazi ya kata.

Wakati huo huo, Mkaguzi Mwandamizi, John Manoti kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Manoti amewataka madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kuwatumikia wananchi - ikiwemo kushughulikia changamoto zinazowakabili.

Kikao hicho cha madiwani kimehudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael mntenjele, miongoni mwa viongozi wengine.

(Imeandikwa na Sauti ya Mara Digital)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages