NEWS

Monday 18 July 2022

Shirika la uhifadhi la FZS lawezesha wanavijiji 6,369 kupata hati miliki za kimila za ardhi SerengetiWANANCHI 6,369 wameanza kupatiwa hati miliki za ardhi za kimila zisizo na kikomo katika vijiji 12 wilayani Serengeti, Mara, kupitia Mradi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Serengeti, unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS), kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Serikali ya Tanzania - kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula, amezindua rasmi ugawaji wa hati hizo (kama inavyoonekana pichani juu) katika kijiji cha Nyichoka kilichopo kata ya Kyambahi, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo, wiki iliyopita.

Waziri Mabula amefafanua kuwa kati ya hati miliki 6,369 zinazotolewa, 1,622 sawa na asilimia 26 zinakwenda kwa wanawake pekee, hati miliki 1,519 (asilimia 25) ni kwa wanaume walioungana na wake zao na 3,228 (asilimia 49) ni kwa wanaume pekee.

Amepongeza Shirika la FZS, wanavijiji na wadau wengine kwa kufanikisha uwekaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, ambayo alisema itasaidia kuvutia wawekezaji, kupunguza migogoro ya ardhi, migogoro ya binadamu na wanyamapori katika vijiji hivyo.

“Ninawapongeza kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo ya ardhi, nimefarijika sana kwa tukio hili. Kitendo cha wanavijiji kupatiwa hati miliki zisizo na kikomo maana yake wamewezeshwa, hivyo mliozipata mzitumie kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kutumia rasilimali ardhi.

“Kwa niaba ya Serikali niwapongeze wenzetu waliofanya kazi hii kubwa kwa kushirikiana na wananchi, kupitia mradi wa Utunzaji na Uendelezaji wa Ikolojia ya Serengeti. Ni safari ndefu mmeanza lakini mmefikia hatua nzuri,” amesema Waziri Mabula.

Meneja Miradi wa Shirika la FZS, Masegeri Rurai (kushoto) akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Waziri Mabula.

Shilingi zaidi ya milioni 800 zimetumika kugharimia utekelezaji wa mradi huo, ambao pia umehusisha uanzishwaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika Vijiji 22 wilayani Serengeti.

Waziri Mabula amesema mbali na faida za kiuchumi na uhifadhi, hatua hiyo itasaidia kumaliza migogoro ya ardhi katika vijiji hivyo.

“Hii haijawahi kutokea na mmewezesha pia mpango wa matumizi bora ya aridhi. Mmefungua milango kwa vijiji vingine mkoani Mara. Kitendo cha kupima tu mmeiongezea ardhi yenu thamani,” amesema.

Amesema sasa wakazi wa maeneo hayo ambayo yapo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wataishi na kufanya shughuli zao za kiuchumi, zikiwemo za kilimo na ufugaji kwa amani.

Amesisitiza kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na wadau wote wa kimaendeleo ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, akitolea mfano Shirika la FZS na Benki ya KfW ya Ujerumani.

“Niwahakikishie kuwa Serikari ya Tanzania haitawangusha katika juhudi hizi za maendeleo kwa Watanzania,” amesema waziri huyo.

Waziri Mabula (wa tatu kushoto waliokaa), viongozi wa wilaya ya Serengeti na wadau wa uhifadhi katika picha ya pamoja siku hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Miradi wa Shirika la FZS, Masegeri Rurai, amesema wananchi zaidi ya 10,000 wanatarajiwa kufurahia matunda yanayotokana na hati miliki hizo za kimila.

“Mpango wa matumizi bora ya ardhi tayari umefikia vijiji 22 na hati miliki 6,369 zinazotolewa katika vijiji 12, ambapo zaidi ya wananchi 10,000 watanufaika nazo,” amefafanua Rurai.

Amesema lengo kubwa la mradi huo ni kuongeza thamani kwa ardhi ya wananchi, kuwainua kiuchumi na kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori, hususan tembo ambao wamekuwa wakiharibu mashamba yao.

Rurai ametaja manufaa mengine ya hati miliki hizo kuwa ni kuzitumia kama dhamana kwenye taasisi za kifedha kama benki na kwenye vyombo vya kisheria.


Waziri Mabula (wa tatu kushoto waliokaa), viongozi wa wilaya ya Serengeti na wahifadhi kutoka TANAPA katika picha ya pamoja siku hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la FZS, Dkt Ezekiel Demba, amesema utekelezaji wa mradi huo umeshuhudia ushurikiano mzuri kutoka kwa TANAPA, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, wananchi na wadau wengine.

Naye Kamishna wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki, ameema mpango huo wa uanzishwaji wa matumizi bora ya ardhi na kuwapatia wananchi hati miliki za kimila, ni muhimu kwa shughuli za maendeleo.

“Hii pia ni nyenzo muhimu katika kumaliza migogoro ya wananchi na wanyamapori,” amesema Kamishna Loibooki.

(Habari na pich zote: Sauti ya Mara Digital)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages