NEWS

Tuesday 26 July 2022

Wakufunzi watumwa kuwanoa wasimamizi, makarani wa sensa Mara



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Salum Hapi.

Na Maximilian Ngessi, Musoma
------------------------------------------

SERIKALI mkoani Mara imewatuma wakufunzi wa sensa ya watu na makazi wa mkoa huo kufikisha kikamilifu maudhui, elimu ya Tehama na miongozo mbalimbali kwa wasimamizi na makarani wa sensa katika wilaya wanazotoka.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi ametoa maelekezo hayo wakati akifunga mafunzo kwa wakufunzi hao wapatao 296 katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare mjini Musoma leo.

Hapi amesema Serikali imetumia fedha nyingi kugharimia maandalizi ya sensa hiyo itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu na kusisitiza wakufunzi hao kuwafundisha wasimamizi na makarani kuwa waadilifu na kutumia kauli inayofaa kwa wananchi.

Amewataka pia kuhimiza wasimamizi na makarani hao kuepuka ubinafsi na tofauti za kisiasa, lakini pia kuhakikisha wanatumia na kutunza vizuri vifaa vyote vya sensa.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya sensa hiyo yako mikononi mwao na kwamba takwimu zitakazopatikana zitaiwezesha Serikali kupanga mipango yake ya maendeleo inayokidhi mahitaji ya wananchi.

Kuhusu changamoto ya vipeperushi vya sensa wilayani, mkuu huyo wa mkoa amesema tayari fedha zimeshatumwa kwa ajili ya kuviandaa.

Awali, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Mara, David Danda amesema mafunzo hayo ya siku 21 yaliyoanza Julai 6, mwaka huu, yamegusa miongozo yote, ikiwemo uadilifu, kuwambia wananchi ukweli na kuwa wavumilivu wakati wa mahojiano na wahusika.

Naye Mwenyekiti wa Sensa wa Wilaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Khalfan Haule ameonya kuhusu matumizi ya simu yasiyofaa kwa wasimamizi na makarani hao kwani yanaweza kuharibu shughuli za kuhesabu watu na makazi.

Wasimamizi na makarani wa sensa zaidi ya 69,000 wanatarajiwa kufikishiwa elimu hiyo katika wilaya zote mkoani Mara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages