Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ya Watu na Makazi Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele.
Na Mara Online News
-----------------------------
KAMATI ya Sensa ya Watu na Makazi Wilaya ya Tarime imeendelea kuimarisha kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiandaa kuhesabiwa siku ya Jumanne Agosti 23, 2022.
Kasi imeongezeka baada ya kikao cha Kamati hiyo kufanyika mjini Tarime asubuhi leo Jumamosi Agosti 20, 2022, kisha wajumbe wake kuwenda kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mji wa Sirari mpakani na nchi ya Kenya.
Katika kikao cha mjini Sirari leo jioni, wajumbe wa Kamati hiyo wamewakutanisha viongozi wa vijiji, mitaa na kata kuwafahamisha maswali yatakayoulizwa ili waweze kusaidia kuhamasisha wananchi wa maeneo yao ya uongozi kutoa ushirikiano na taarifa sahihi kwa makarani wa sensa.
Viongozi wa vijiji na mitaa kikaoni mjini Sirari
“Kampeni inaendelea vizuri na tunapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa vijiji, vitongoji, kata na wananchi kwa ujumla,” Mratibu wa Sensa Wilaya ya Tarime, Modest Lema ameiambia Mara Online News na kuongeza kuwa Kamati hiyo inazunguka mijini na vijijini kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu.
Naye mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo, Jacob Mugini amesema wanawashirikisha kwa karibu viongozi wa ngazi hizo kwani wana nafasi kubwa ya kusaidia kufanikisha sensa hiyo.
Mjumbe wa Kamati ya Sensa Wilaya ya Tarime, Jacob Mugini (kulia) akizungumza katika kikao cha uhamasishaji mjini Sirari.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sirari, Wakuru Mirumbe na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buriba, Ambrose Wantaigwa, wamesema uhamasishaji wa sensa unaendelea vizuri katika maeneo yao ya uongozi, wananchi wameelimishwa na wako tayari kuhesabiwa.
Kesho Kamati ya Sensa Wilaya ya Tarime inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Kanali Michael Mntenjele, itaendelea na uhamasishaji zaidi katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo Rebu na Nyamongo.
No comments:
Post a Comment